WANACHAMA wa Kishindo cha Mama kwa kushirikiana na TOGABE Mills watoa Msaada kwa waathirika wa Mafuriko Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.

Wametoa misaada mbalimbali ya kibinadamu vikiwemo Unga, Maharage, Mchele, Mafuta ya Kupikia pamoja na nguo.
MKuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele (Watano kutoka kushoto) Wanachama wa Kishindo cha Mama na TOGABE Mills wakiwa katika picha ya pamoja wakiwa na vyakula vilivyotolewa waathirika wa Mafuriko Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.

Baadhi ya wanakibiti wakisaidia kushusha baadhi ya misaada iliyotolewa na Wanachama wa Kishindo cha Mama na TOGABE Mills mara baada ya kutolewa walipotembelewa na wanachama hao.
MKuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele na Wanachama wa Kishindo cha Mama na TOGABE Mills wakiondoka na vyakula vilivyotolewa waathirika wa Mafuriko Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.



MKuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele (Wapili kutoka kushoto) akizungumza na Wanachama wa Kishindo cha Mama na TOGABE Mills mara baada ya kukabidhi msaada kwa waathirika wa Mafuriko Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.

MKuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele akiwa na Tisheti aliyopewa na wanachama wa Kishindo Cha Mama.
Wanachama wa Kishindo cha Mama na TOGABE Mills wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kutoa Msaada kwa waathirika wa Mafuriko Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.

Picha ya pamoja.

MKuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhiwa misaada na Wanachama wa Kishindo cha Mama na TOGABE Mills vilivyo kwa waathirika wa Mafuriko Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.
Afisa Masoko wa TOGABE Mills, Ramadhan Kimomwe akizungumza na waandishi mara baada ya kutoa msaada kwa waathirika wa Mafuriki Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.

*Wakumbushwa kutekeleza majukumu yao bila kuathiri afya zao

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

KATIBU Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu Mwamba amewapongeza wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Taasisi zake kwa kujisimamia vyema katika utekelezaji wa majukumu kwa kufuata miongozo ya Serikali na kuwataka kuendelea kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miiko ya utumishi wa Umma pamoja na kujali usalama wa afya zao kwa kufanya mazoezi, kupata lishe bora pamoja na kupima afya zao.

Akizungumza Leo jijini Dar es Salam wakati akifungua Mkutano wa 37 wa mwaka 2023/2024 wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Fedha Dkt. Natu Mwamba amesema katika kuboresha huduma kwa wananchi na wadau wa Fedha ni lazima kazi zifanywe kwa ubunifu na ushirikiano wa Wizara, idara, vitengo na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo nyeti na muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Nchi.

“Niwapongeze kwa utendaji kazi wa Wizara ya Fedha na taasisi zake kupitia Government Structure inavyotekeleza majukumu yake sipati malalamiko ya moja kwa moja kuhusu Wizara yetu, Nawapongeza wakuu wa Taasisi na bodi za wakurugenzi na wafanyakazi kwa kujiendesha vyema chini ya bodi…..Wizara ya Fedha tupo vizuri taasisi zinajisimamia vizuri sana.” Amefafanua.

Amesema baraza la wafanyakazi ni jukwaa muhimu la majadiliano mahali pa kazi lililoundwa kwa mujibu wa Sheria na kuipongeza Wizara hiyo kwa kutekeleza takwa hilo la kisheria la kuunda baraza la wafanyakazi ili kutoa fursa ya majadiliano ya masuala ya ajira na mazingira ya kazi baina ya mwajiri na mwajiriwa.

“Baraza la Wafanyakazi ni chombo muhimu cha ushirikishwaji wa wafanyakazi katika maamuzi muhimu yanayohusu uendeshaji na utendaji wa Wizara…..Nasisitiza na kuelekeza kuwa ni lazima tuzingatie matakwa ya kisheria ya kufanya mkutano wa baraza la wafanyakazi na nipate taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya baraza kila tunapofanya mkutano kwa kuwa kupitia mikutano hii tukiwa taasisi nyeti tunapata fursa ya kuzungumza na kupanga mikakati bora ya kutoa huduma kwa wananchi na wadau wetu.” Amesema.

Aidha amesema kuwa, Hoja zitakazojadiliwa katika mkutano huo zilenge kuboresha mazingira ya kazi, mifumo ya usimamizi na mipango wa Wizara na huduma kwa wadau wa ndani na nje.

“Katika kupiga hatua zaidi niwahakikishie kuwa Ofisi yangu ipo wazi kwa majadiliano ya hoja zote za kiutumishi, kiutawala na kiutendaji ili kuboresha mazingira ya utendaji kazi na huduma kwa wadau wetu…..Pia ni muhimu kuandaa programu za mafunzo ya masuala ya kitaaluma, kitaalam, maadili na umahiri mahala pa kazi na pia tuzingatie mabadiliko mbalimbali yanayoendelea kutokea katika mifumo ya usimamizi wa fedha, mipango, uchumi, utawala bora na mazingira hii italeta chachu katika kutekeleza majukumu kwa weledi, ubunifu na uadilifu.” Ameeleza.

Kuhusiana na suala la afya Dkt. Natu amewataka wajumbe wa mkutano huo kutekeleza majukumu yao bila kuathiri afya zao kwa kutenga muda kwa ajili ya mazoezi, kuzingatika lishe bora na kupima afya mara kwa mara kwa kuwa maisha ya utumishi bila magonjwa sugu inawezekana.

“Niwapongeze watumishi 301 wa Wizara ya Fedha waliojitokeza katika zoezi la uelimishaji na upimaji wa magonjwa sugu yasiyoambukiza mahali pa kazi Mwezi huu Aprili, watumishi 179 walikuwa wanawake sawa na asilimia 56.5 ya watumishi wote waliojitokeza na wanaume walikuwa asilimia 43.5 na watumishi hao walipata elimu na kupima sukari, msukumo wa damu, macho, afya ya akili na UKIMWI.” Amesema.

Ameeleza kuwa takwimu zinaonesha kuwa wengi wanakabiliwa na matumizi makubwa ya sukari, chumvi na mafuta kuliko mahitaji pamoja kutopata muda wa kupumzika hali inayopelekea wengi kuwa na uzito uliopitiliza na kuwashauri kuzingatia taratibu za afya wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Hazina Scholastica Okudo amesema kuwa mkutano huo unafanyika kila mwaka kwa mujibu wa Sheria na Wizara imekuwa ikitumia fursa hiyo kukutana na kujadili masuala mbalimbali kwa lengo la kuboresha huduma wanazozitoa kwa wananchi na wadau mbalimbali na kuchochea uchumi wa Taifa.

Amesema Wizara ya fedha imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa uwazi na utawala bora hali inapelekea utekelezaji wa urahisi katika kuziba mianya ya rushwa.

Katika mkutano huo wa siku mbili wajumbe wao watapata fursa ya kujadili mada mbalimbali ya Wizara hiyo ili kuendelea kuleta matokeo chanya kwa Taifa.  

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu Mwamba akizungumza wakati akifungua Mkutano wa 37 wa mwaka 2023/2024 wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Fedha leo Aprili 24,2024 Jijini Dar es Salaam













 

Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU), Dkt. Paul Loisulie,akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Uchambuzi na Mapendekezo ya hoja za NHIF na Pensheni nchini Tanzania.
Na Mwandishi Wetu

KUELEKEA Bima ya Afya kwa Wote Chama Cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu (THTU) imeshauri serikali kuendelea kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaotumia vibaya fedha za mifuko ya bima ya afya ili kukomesha tabia hiyo.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa THTU Taifa Dk. Paul Loisulie, wakati akitoa Mapendekezo ya Hoja Za NHIF na Pensheni Nchini Tanzania.

Alisema pamoja na changamoto zote na dalili isiyo nzuri juu ya Bima ya Afya kwa wote, THTU inaamini kuna mambo ya kufanyika kwa utashi sahihi na nia thabiti ili kuwezesha Bima ya Afya kwa wote ifanye kazi kwa ufanisi mkubwa.

“Serikali iwe na hasira na wivu juu ya rasilimali zinazotapanywa kila mara katika mifuko hii na kuchukua hatua ya kukomesha.

Aliongeza kuwa :”Isisubiri ripoti ya CAG bali ichukue hatua mapema. Serikali pia iepuke utaratibu wake wa kukopa au kujichotea pesa kutoka kwenye mfuko ili pesa hizo zitumike kugharamia huduma za afya tun a si vinginevyo,”

Loisulie alishauri Bunge litimize wajibu wake kikamilifu katika kutunga sheria rafiki kwa wafanyakazi na wanajamii Pamoja na kuisimamia serikali katika usimamizi wa mifuko husika.

Alisisitiza kuwa Bunge halipaswi kuwa sehemu ya kulalamika bali kutatua changamoto zinazojitokeza

Katika hatua nyingine alisema upo ulazima wa Wafanyakazi, wanajamii na wanufaika wote wa Bima kuamka usingizini na kuacha tabia ya kugugumia chini kwa chini huku Mfuko ukiteketea.

“Ijengeke tabia ya kuhoji na kushinikiza uwajibikaji pale matumizi mabaya na usimamizi usioridhisha inapobainika na mamlaka zinazoaminika kama CAG,”alifafanua .

Aliongeza kuwa :” Ifanyike mijadala ya wazi na shirikishi kuhusu uhai wa mfuko mara kwa mara ili kubaini changamoto na namna ya kuzitatua badala ya kuachia mfuko peke yake. Hii itahusisha pia kutumia ripoti za kitaalamu za tathmini juu ya mwenendo wa mfuko,”.

Kuhusu Kikokotoo, (THTU) imependekeza Kikokotoo kifanyiwe mabadilko kwa kuongeza umri baada ya kustaafu toka miaka 12.5 hadi 15.5 na wanachama wapewe angalau 50% kama mafao ya mkupuo.

amesema "Kuhusu hoja ya Kikokotoo kinachotumika hakiakisi hali halisi ya wanachama – kanuni 8(1)(a)(b)(c) (a) kigezo cha umri (b) kigezo cha malipo ya mkupuo mapendekezo yao ni Kikokotoo kifanyiwe mabadilko kwa kuongeza umri baada ya kustaafu toka miaka 12.5 hadi 15.5."amesema Dkt.Loisulie
Pia wanachama wapewe angalau 50% kama mafao ya mkupuo itumike 1/540 badala ya 1/580.
Kuhusu Waziri husika kuwa na mamlaka ya kuamua kiwango cha michango ya mwanachama katika mfuko wanapendekeza Kifungu kidogo cha 18(2)(b) kiondolewe.
Na WILLIUM PAUL, MOSHI.

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amekabidhi magari matatu kwa ajili ya wakuu wa wilaya za Rombo, Mwanga na Same ili kuongeza ufanisi wa utendaji na kuleta maendeleo ya mkoa yenye thamani ya zaidi ya milioni 200.

Akizungumza katika hafla fupi ya makabidhiano hayo nje ya viwanja wa ofisi za mkuu wa mkoa, Babu amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameanza kutekeleza maombi mbalimbali ya mkoa wa Kilimanjaro ya kuwapatia Wakuu wa wilaya vitendea kazi.

Babu alisema kuwa, Wabunge wamekuwa wakilalamika Bungeni kuhusiana na wakuu wa wilaya kukosa magari ambapo mkoa ulipanga kuhakikisha bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 mpaka ifikapo mwezi Juni mwaka huu wawe wameshanunua magari matatu ya wakuu wa wilaya.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa, magari hayo yatatumika kwa ajili ya shughuli za kiserikali na kuwataka kwenda kuyatunza magari hayo kwani yamenunuliwa kwa gharama.

Aidha Babu amewataka Wakuu wa wilaya kuwaachia Madereva wafanye kazi zao kwani ndio waliyosomea kuendesha gari na kuachana na kumwambia kuvunja sheria ili kuwahi kule unapoenda ili kuepuka ajali zisizo na ulazima.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Rombo, Raymond Mangwala alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali wasaidizi wake na kuwapa vitendea kazi na kuahidi kutumia gari hilo kufanya kazi iliyokusudiwa ikiwemo kuhakikisha miradi inaenda kukamilika.

Naye mkuu wa wilaya ya Same, Kasilda Mgeni alisema kupatikana kwa vitendea kazi kutachangia kuwafikia wananchi na kutatua kero zao .




Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel John Nchimbi akipunga mkono kuwaaga mamia ya wananchi, walioongozwa na viongozi wa chama na Serikali Mkoa wa Ruvuma, waliofika Uwanja wa Ndege wa Songea, kumuaga kiongozi huyo baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani humo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku 13 iliyomfikisha katika mikoa sita, akianzia Katavi, kisha Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Ruvuma.

Balozi Nchimbi, ambaye katika ziara hiyo aliambatana na Issa Haji Usi Gavu, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Oganaizesheni na Amos Gabriel Makalla, Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, akiwa ziarani kwenye maeneo mbalimbali ya mikoa hiyo, amekagua na kuhamasisha uhai na ujenzi wa chama.

Aidha, katika ziara hiyo pia, Balozi Nchimbi ametoa maelekezo mbalimbali kwa baadhi ya viongozi na watendaji wa wizara yaliyolenga kuboresha na kuongeza kasi ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020 - 2025, hasa maeneo ya miradi ya maendeleo ya wananchi na kuwatumikia watu.

Kupitia ziara hiyo, CCM katika ngazi ya taifa, hasa kupitia kwa Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, imeendeleza utaratibu wake wa kusikiliza kero za wananchi na kuzitolea maelekezo kwa ajili ya kuzitatua, huku Gavu akiendelea kuhamasisha wanachama na viongozi kuendelea kukiimarisha CCM na kujiandaa kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (2024) na Uchaguzi Mkuu (2025).








Na Khadija Kalili,Michuzi TV
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani imefanya uchambuzi wa mfumo wa ukusanyaji wa mapato yatokanayo na machinjio ya Mtakuja iliyopo Halmashauri ya Mji Kibaha .

"Uchambuzi huu umefanywa baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba kuna miaya ya rushwa katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na ushuru katika machinjio hayo,hali inayodababisha upotevu wa mapato na Halmashauri hiyo hivyo kushindwa kufikia lengo la

ukusanyaji waliyojiwekea kutoka kwenye chanzo hiki" amesema Kaimu Kamanda TAKUKURU Mkoa wa Pwani Ally Sadiki alipozungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari ambao umefanyika leo Aprili 24.

"Uchambuzi huu umebaini kwamba, pamoja na kuwepo kwa mashine za kieletroniki za POS katika machinjio kumekua na taarifa zinazokinzana ,kuwepo kwa tatizo la miundombinu na ucheleshaji wa kuweka fedha benki zinazo kisanywa.

TAKUKURU imebaini pia kuna uzembe katika kusimamia idadi ya ng'ombe wanao chinjwa kwa siku husika na hakuna ukaguzi kuhusu idadi ya ng'ombe waliopo eneo la kusibiri kuchinjwa.

"TAKUKURU imebaini kuwa idadi ndogo ya watumishi walioajiriwa eneo husika ndiyo chanzo cha kushindwa kutekeleza majukumu ipasavyo"amesema Kaimu Kamanda TAKUKURU Sadiki.

Aidha amesema kuwa baada ya TAKUKURU kuingilia kati makusanyo yameongezeka tofauti na ilivyokua katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita kati ya Oktoba na Desemba 2023 ambapo Oktoba hadi Desemba makusanyo yalikua Mil.7,418,000 na sasa makusanyo yameongezeka na kufikia kiasi cha Mil.9,615,000.

"Katika hatua ingine Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha Mji ameongeza watumishi eneo hilo la machinjio ya Mtakuja kuimarisha ufuatiliaji na ukaguzi hivi sasa unafanyika kila mara ili kuondoa fedha za makusanyo ya kila siku na kuhakikisha fedha zinapelekwa benki kila siku.

Kaimu Kamanda wa TAKUKURU amesema kuwa kwa kipindi tajwa wamefanya chambuzi nyingine za mifumo tano katika sekta ya Ardhi,Elimu, AMCOS na ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya serikali ili kupata tija ya mifumo imara usiyokwamisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Ameongeza kwa kusema kuwq TAKUKURU Mkoa wa Pwani wamefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 23 yenye thamani ya Bilioni6.3 katika sekta za Elimu, Maji,Afya na Ujenzi (Barabara),ambapo kati ya miradi hiyo mradi mmoja umeonekana kuwa na upungufu ufuatiliaji u aendelea ii kurekebisha kasoro hizo.

Kaimu Kamanda TAKUKURU Mkoa wa Pwani Sadiki amesema kuwa katika kipindi hicho cha miezi mitayu wameweza kutoa elimu kwa umma kwa kufanya semina 19,mikutano yahadhara21,

vipindi vya redio 9 kuimarisha klabu za wapinga rushwa 54 uandishi makala 4 na TAKUKURU Rafiki6.

Aidha TAKUKURU Mkoa wa Pwani imefungua kesi mpya mbili Mahakamani ambapo kesi sita zimeamuliwa huku kesinne watuhumiwa wametiwa hatiani na jumla kesi sita zinaendelea Mahakamani.

Ameongeza kwa kusema kuwa mikakati waliyojiwekea ni kwamba wamejipanga kuendelea kufanya udhibiti wa mapato ya serikali na usimamizi wa rasilimali za umma ikiwa ji pamoja na udhibiti wa fedh zinazotolewa na serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze, April 24
NAIBU Waziri wa Utumishi na Utawala Bora ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze ,Ridhiwani Kikwete amewataka wanafunzi na vijana kuacha matumizi mabaya ya mitandao, mambo yaliyo nje ya tamaduni za kitanzania na badala Yake watumie mitandao hiyo kujifunza na kujipa uelewa zaidi katika masuala ya masomo na elimu.

Aidha amewaasa kusoma kwa bidii kwani elimu ndio nguzo ya maisha yao.

Ridhiwani alitoa rai hiyo alipokuwa akihutubia wahutimu wa kidato cha sita shule ya sekondari ya Lugoba , Halmashauri ya Chalinze, mkoani Pwani.

Aliwaasa wahitimu hao kuhakikisha wanafaulu ili waache deni la kufuatwa na wadogo zao wanaowafuata kwa upande mmoja, wawape heshima walimu na wazazi kwa kufaulu vizuri.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo ,Abdallah Sakasa aliishukuru serikali kwa kuendelea kupeleka pesa za elimu bure , vifaa na kuongezeka kwa madarasa na walimu shuleni hapo .

Alimuomba mbunge kuendelea kuikumbuka shule hiyo kwa kuisaidia vifaa na kuongeza mabweni ya wanafunzi.





RAIS Samia Suluhu Hassan Atunuku Nishani Viongozi Mbalimbali katika shamrashamra za miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimtunuku na kumvalisha Nishani ya Mwenge wa Uhuru Daraja la Pili Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Awamu ya Tatu Mhe. Fredrick kwenye hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 24 Aprili, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimtunuku na kumvalisha Nishani ya Mwenge wa Uhuru Daraja la Pili Makamu Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mohamed Gharib Bilal kwenye hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 24 Aprili, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimtunuku na kumvalisha Nishani ya Mwenge wa Uhuru Daraja la Pili Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Samwel Malecela kwenye hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 24 Aprili, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Mama Janeth Magufuli Nishani ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo aliipokea kwa niaba ya Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwenye hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 24 Aprili, 2024. Nishani ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hutunukiwa kwa Wakuu wa Nchi Wastaafu (hai au marehemu) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walioingia madarakani kwa njia ya kikatiba na wameendelea kuonesha Maadili mema yenye nidhamu, heshima na mfano wa kuigwa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Mama Salma Kikwete Nishani ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo aliipokea kwa niaba ya Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwenye hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 24 Aprili, 2024. Nishani ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hutunukiwa kwa Wakuu wa Nchi Wastaafu (hai au marehemu) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walioingia madarakani kwa njia ya kikatiba na wameendelea kuonesha Maadili mema yenye nidhamu, heshima na mfano wa kuigwa.

Top News