Na Bashir Yakub
Nimewahi kuandika mara kwa mara kuhusu utaratibu mzuri wa kumwezesha mtu kununua nyumba huku akiwa ameepuka mgogoro. Nilitahadharisha sana kuhusu migogoro ya ardhi ambayo sasa imekuwa janga la kitaifa hapa kwetu. Nakumbuka moja kati ya mambo niliyoeleza ni kuwa utaratibu wa manunuzi ya nyumba/viwanja unatofautiana.Nikasema kwamba tofauti zake zinatokana na ukweli kuwa kila nyumba ina mazingira yake. Hata hivyo sikusema utofauti wa mazingira hayo ila sasa naweza kueleza kwa ufupi utofauti wa mazingira ya kila nyumba unapokuwa katika taratibu za ununuzi.
1.UTOFAUTI WA KITAALAM KATIKA UNUNUZI NYUMBA.
Usikurupuke unapohitaji kununua ardhi. Unapaswa kujua kuwa nyumba na viwanja zina taratibu tofauti unapohitaji kununua. Ukikurupuka utalipia gharama ya kukurupuka kwako. Kutokana na hilo ni muhimu tujue kuwa kuna nyumba inayouzwa kwa utaratibu wa kawaida wa mmiliki mwenyewe kumuuzia mnunuzi. Hii mara nyingi huwa haina shida sana kwakuwa unahitaji tu kujiridhisha na baadhi ya mambo ya msingi kama kufanya upekuzi rasmi ( official search) katika mamlaka za ardhi n.k.
Pili kuna nyumba inayouzwa na wasimamizi wa mirathi. Hii uuzwaji wake hauko sawa na ile inayouzwa na mmiliki halisi. Hawa ni wasimamizi wa mirathi hivyo hata uuzaji wao si uuzaji kama wa mmliki halisi. Utofauti wao upo katika namna ya kuandika mkataba( sale agreement) na nyaraka ambazo wanapaswa kukuonesha wewe mnunuzi . Pia kuna ununuzi wa nyumba ya mkopo ambao sasa ndio mada ya leo. Ununuzi wa nyumba ya mkopo nao si ununuzi kama wa nyumba ya kawaida. Haufanani na nyumba ya kawaida na haufanani na wa nyumba ya mirathi. Unazo tarati bu zake tofauti kabisa na ununuzi mwingine.
2.UMUHIMU WA KUZINGATIA UTARATIBU UNAPONUNUA NYUMBA YA DHAMANA.
Tatizo kubwa linakuja kuwa unaponunua bila kuzingatia utaratibu pia uwe tayari kupoteza. Ieleweke kuwa nyumba au ardhi yoyote ni kitu ambacho hudumu milele. Hivyo kama utakosea utaratibu hata kwa kiwango kidogo basi ya kutosha kuishi bila amani maisha yako yote. Kama si wewe watakuwa watoto wako na kama si watoto wako watakuwa wajukuu wako. Kati ya hawa kuna mmoja mgogoro utamkuta kwa makosa uliyoyafanya wewe. Na ubaya wa mgogoro unapotokea mahakama kikubwa inachokifanya ni kuangalia nani alikosea taratibu. Inaangalia hilo kwasababu yenyewe inakuwa haipo wakati mnauziana na hivyo nyote haiwajui na haijui kati yenu nani mkweli na nani muongo.
Kwahiyo kama ni wewe mnunuzi uliyekosea taratibu wakati wa kununua basi hakuna kingine ila kupoteza bila kujali gharama ulizotumia katika manunuzi. Lakini ikiwa ulifuata taratibu kwa umakini kwanza ni vigumu kuingia katika mgogoro lakini hata bahati mbaya uingie katika mgogoro basi ushindi utakuwa ni wa kwako. Huu ndio umuhimu wa kuhakikisha unafuata taratibu. Zingatia maeneo mawili kwanza uandaaji wa mkataba na pili ukaguzi na uhakiki wa nyaraka.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...