Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Machi 3, 2015, ameungana na mamia ya waombolezaji kumzika Mbunge wa Jimbo la Nyasa na msanii mahiri wa muziki nchini, Mheshimiwa Kepteni John Damiano Komba, kwenye makaburi ya Kanisa Katoliki katika Kijiji cha Lituhi, Wilaya ya Nyasa, Mkoa wa Ruvuma. 
Mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Songea, akitokea Dar es Salaam, kiasi cha saa tano na robo asubuhi, Rais Kikwete amekwenda moja kwa moja Lituhi, karibu kiasi cha kilomita 140 kutoka mjini Songea, kwa ajili ya mazishi ya Mheshimiwa Komba ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM). 
Rais Kikwete amejiunga na waombolezaji akiwemo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anne Semamba Makinda kiasi cha saa tisa mchana kwa ajili ya mazishi ya mmoja wa wasanii ambao walijijengea heshima kubwa kwa nyimbo zake za uhamasishaji. 
Wakati wa shughuli za mazishi ambazo kidini zimeongozwa na Askofu John Ndimbo wa Jimbo Katoliki Mbinga, waombolezaji walisomewa salamu za rambirambi ambazo zimetumwa na Rais wa Pili wa Malawi, Mheshimiwa Bakili Muluzi ambaye sasa amestaafu. 
Katika salamu hizo, Mheshimiwa Muluzi amesema: “Nilimjua Komba kama rafiki na taarifa za kifo chake cha ghafla zimenistua sana.” 
Mwili wa Marehemu Komba uliteremshwa kaburini saa 9:30 mchana huku ukishuhudiwa na mjane wa marehemu Salome Komba na watoto wake 11. 
Rais Kikwete ameondoka Lituhi mara baada ya mazishi kurejea mjini Songea kumalizia ziara yake ya siku mbili ya kikazi mkoani Ruvuma.
Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo la Mbinga Mhashamu John Ndimbo akiongoza ibada ya mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Mbinga Magharibi marehemu Kapteni John Damiano Komba wakati wa ibada ya mazishi yake yaliyofanyika kijijini kwake Lituhi wilayani Nyasa Mkoani Ruvuma leo.(picha na Freddy Maro).
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakiweka udongo katika kaburi la aliyekuwa mbunge wa Mbinga Magharibi marehemu Kapteni John Damiano Komba wakati wa ibada ya mazishi yake yaliyofanyika kijijini kwake Lituhi wilayani Nyasa ,Mkoani Ruvuma.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakiweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa mbunge wa Mbinga Magharibi marehemu Kapteni John Damiano Komba wakati wa ibada ya mazishi yake yaliyofanyika kijijini kwake Lituhi wilayani Nyasa ,Mkoani Ruvuma. Habari na picha na IKULU.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 12 mpaka sasa

  1. Mimi ni m-Katoliki. Napenda kusema kuwa kwenye ibada kama hii, hizi kofia zinazoonekana pichani si mahala pake. Zimenikera. Kofia ya askofu ni mahala pake, ni sehemu ya mavazi yake rasmi wakati wa ibada. Kama wa-Katoliki wenzangu wanaona nimekosea, wana wajibu wa kunikosoa.

    ReplyDelete
    Replies
    1. hapa hukosolewi bali unafundishwa ili siku nyingine utumie busara kabla kuandika upuuzi wako .naamini wewe ni mkatoliki na unaijua sana dini yako ya kikatoliki toa ushahidi kutoka kwenye kitabu chako cha kikatoliki kinasema ni dhambi kuvaa kofia kwa asiye askofu wakati wa maziko

      Delete
  2. Mheshimiwa Mbele uko karibu na ukweli japo hapo walipo ni makaburini na sio kanisani!! Isitoshe, Marehemu Komba (RIP) alikuwa mtu wa CCM na hao kama washirika wenzake katika chama walilazimika kumzika ki chama; kiitikadi ya chama chao. Sidhani kama kuna tatizo lolote!!

    ReplyDelete
  3. Pole ndugu yangu Mbele, misiba siku hizi inatumika kama majukwaa ya kisiasa. Hakuna anayejali wafiwa au kutoa heshima kwa wana familia au viongozi wa dini. Watu wanaangalia malengo yao ya kisiasa ndugu.

    ReplyDelete
  4. Ndugu Mbele mie si Mkatoliki kama ulivyotaka Wakatoliki tu ndio wakukosoe. Kwanza umeonyesha udini sana katika jambo hili, hayo ni makosa kwa Mtanzania rejea wosia wa Baba wa Taifa. Pili jiulize kwani hapo ni ndani ya Kanisa? Hapo ni makaburini kila mtu na dhehebu lake anahudhuria na hata asiye na dini pia.

    ReplyDelete
  5. Mdau hapo juu amemkumbusha vyema kabisa Bw. Mbele. Tusizungumzie udini hapa ni wakati wa majonzi na ni vyema tukatoa heshima kwa marehemu ni uungwana tu katika hili na si mabishano. Nadhani pia rangi za kofia zinang'aa sana kiasi Bw. Mbele kaziona zaidi kuliko tukio zima.

    ReplyDelete
  6. Hivi ni nafsi ndio inayowatuma kukosea dini au kuna nafsi chafu imetawala mioyoni mwenu ambao inawatuma kukosoa dini?? Ni nani ambae alisema hii inafaa pale lakini haifai hapa??

    Binafsi sioni tatizo ya Kofia...

    Elimu mlizonazo zisifanye mkahoji maswala ya dini, imani au Mungu...Wacheni imani ziwe imani, Dini ziwe dini na Mungu abaki Mungu na elimu zenu za Uprofesa au Udaktari zibaki kuwa hivyo hivyo..

    Asanteni sana kwa kunisoma kwani nami haya ndio mawazo yangu na Mungu awabariki sana.

    ReplyDelete
  7. Mimi nimejieleza kwa dhati kutokana na nilivyolelewa katika dini yangu. Ninavyoelewa, mazishi ya ki-Katoliki ni Ibada, na yana taratibu zake. Sikuleta duku yangu kama mzaha. Sichukulii imani au ibada ya dini yangu kama mzaha. Sichukulii imani au ibada au ibada ya dini yoyote kama mzaha.

    Nina haki ya kuwaomba wa-Katoliki wenzangu wanielimishe, iwapo nimeshindwa kulielewa suala hili linalihusu ibada ya mazishi ya ki-Katoliki. Sijafanya udini.

    Mimi mwenyewe ninaziheshimu dini za wengine na ibada zao. Siwezi kujiingiza katika mazungumzo yao ya ibada zao kama alivyojiingiza huyu anonymous hapa juu ambaye ametamka kuwa si m-Katoliki. Sielewi ana lengo gani kuingilia suala linalihusu ibada na ibada ya dini yangu. Namwomba akae kando.

    Nimewahi kuhudhuria mazishi ya ki-Islam. Nikiwa pale, ninahakikisha nimefuata taratibu zote zinazotakiwa, na mara ya kwanza kuhudhuria ilikuwa ni sehemu fulani pale Dar es Salaam, ambapo mfiwa aliyenialika ni rafiki yangu Dr. Tigiti Sengo. Ndipo nilipoanza kupata uzoefu wa ibada za mazishi ya ki-islam. Siwezi kuleta maneno kama haya niliyosoma hapa juu dhidi ya imani au ibada za dini nyingine.

    Kuheshimiana ibada na imani za dini si udini. Udini ni kuwadhulumu, kuwabagua, au kuwapendelea watu kwa kigezo cha dini, badala ya kuwarendea haki.

    Narudia ombi langu kwa wa-Katoliki wanaoweza kunielimisha kuhusu suala la zile kofia kwenye ibada ya mazishi ya ki-Katoliki.

    ReplyDelete
  8. Hayo ya kofia sio ya msingi sana. Kama mkatoliki nafahamu mazingira kama haya ya imani mchanganyiko, mavazi mchanganyiko n.k. hakuzuii ibada kufanyika kwani walengwa wa ibada wanafahamika. Kinachokera sana ni wanasiasa kuteka matukio, hasa misiba na harusi za wakubwa! Wao ndio wanakuwa wazazi na ndugu zaidi ya wahusika halisi!

    ReplyDelete
  9. Mh Mbele kubali umechemka kwenye ili swala na jaribu kuweka pembeni elimu yako na maswala ya imani, udini na Mungu...Hapa umesema wazi wazi kuhusu kofia na kwamba umechukizwa na hiyo kofia na ata kama ungehitaji kuelimishwa kuhusu kofia basi ungeomba kuelimishwa na kuuliza swali na SIO kuponda maswala ya imani au dini na kuonesha chuki ktk mavazi ya kidini!

    au elimu yako na kukaa nje ya nchi saaaana kumekufanya uone imani, dini na haya maswala ya Mungu ni maswala ambayo SIO na yanakukera??! Au kuna roho mchafu kwenye nafsi yako ambae ndie anakutuma?

    Mungu akubariki na akuokoe mapema, tukifika uzeeni na magonjwa kutufuata mara kwa mara basi hapo ndio tunajifanyaga kujua imani, dini na kumkumbuka Mungu siku zote. Amka sasa.

    ReplyDelete
  10. Nilichofanya ni kuelezea kuwa nimekerwa na kitendo cha watu kuvaa hizo kofia wakati wa mazishi ya ki-Katoliki. Sikuishia hapo, bali, kwa kutambua kuwa huenda sielewi vizuri masherti ya ibada ya mazishi ya ki-Katoliki, nimewaomba wanaojua wanielimishe.

    Ni kauli ambayo si ngumu kuielewa. Hilo suali langu linahusu imani na ibada ya dini yangu. Mbele ya dini au mbele ya Mungu, hakuna mambo ya uprofesa. Tuzingatie hilo.

    Nimeelezea jinsi ninavyoheshimu imani na ibada za dini zote. Lakini bado nazushiwa mambo kinyume. Naambiwa ninaponda masuala ya imani na dini.

    Sijui ni wapi nimefanya hivyo, wakati duku duku yangu ilijengeka katika kutafuta uhakika kuwa ibada ya mazishi imefanyika ipasavyo, kwa mujibu wa ibada zetu, kama namna ya kuheshimu ibada na kumheshimu marehemu.

    Ni heri watu wangeniuliza nina maanisha nini, badala ya kunipakazia na kunizulia mambo ambayo sikuyasema, wala hayakuwemo mawazoni mwangu.

    Mkijiita "anonymous," mimi siwezi kuwatambua, lakini kumbukeni kuna Mungu. Mtajulikana siku ya kiyama.

    Duku duku yangu kuhusu zile kofia wakati wa mazishi ya ki-Katoliki bado haijajibiwa. Ninalihamishia suali langu kwenye blogu yangu: http://www.hapakwetu.blogspot.com

    ReplyDelete
  11. Mtu akisema kwamaba taratibu za ibada zifuatwe pale tu watu wanapo kuwa makanisani ni kukosea. Taratibu za ibada zinatakiwa kufuatwa sehemu yoyote watu wanapofanyia ibada iwe kanisani au chini ya mti. na nyie wana CCM kuwani na heshima maana kama mlikuwa mnamsindikiza mwenzenu kwa uniform hata T-shirt pekee inajulikana kuwa ni ya CCM siyo mpaka kofia. Heshimuni ibada aijalishi ni ya thehebu gani. Ni hayo tu

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...