Na Ramadhani Ali –Maelezo Zanzibar 
Waislamu wa Zanzibar wanaotegemea kutekeleza Ibada ya Hijja mwaka huu wameshauriwa kukamilisha mipango ya safari hiyo mapema ili kuziwezesha Taasisi zinazosafirisha mahujaji kuweza kukamilisha taratibu mpya zilizowekwa na Serikali ya Saudi Arabia. 
Akizungumza katika Kongamano la mahujaji watarajiwa lililofanyika ukumbi wa Beit al Yamin Malindi, Afisa kutoaka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Ustaadh Khalid Mohammed Mrisho amesema Serikali ya Saudi Arabia imefanya mabadiliko makubwa ya taratibu za maandalizi ya Hijjah kuanzia mwaka huu. 
Amesema wamefanya maamuzi hayo baada ya malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na mahujaji kutokana na vitendo vya udanganyifu vilivyokuwa vikifanywa na baadhi ya Taasisi zinazosafirisha mahujaji kutoka mataifa mbali mbali duniani. 
“Baadhi ya viongozi wa Taasisi zinazosafirisha mahujaji walikuwa wakiwatoza fedha mahujaji wao kwa ajili ya kulipia Viwanja vya ndege vya Makka na Madina lakini walikuwa hawalipi na mahujaji kuzuiliwa kwa saa kadhaa,”alisema Ustaadh Khalid. 
Taasisi nyengine alisema zilikuwa zinawaahidi mahujaji kuwakodia nyumba nzuri za karibu katika miji mitakatifu ya Makka na Madina lakini wanapofika huko huwekwa kwenye nyumba mbovu na wengine hukosa huduma ya chakula. Amesema katika kukabiliana na matatizo hayo Serikali ya Saudia Arabia kuanzia sasa imeziagiza Taasisi zinazosafirisha mahujaji kufanya taratibu zote za maandalizi ya safari, makaazi na matembezi kwa njia ya mtandao na kulipa gharama zote wakiwa nchini mwao. 
Amesema iwapo taratibu hizo hazikukamilika hujaji atakosa visa ya kuingia Saudi Arabia na atakuwa amekosa kutekeleza ibada ya Hijjah kwa mwaka huo. Ameongeza kuwa mwaka huu nchi hiyo imeweka hadi tarehe 27 Juni kuwa ni siku ya mwisho kukamilisha taratibu za mahujaji na baada ya tarehe hiyo mtandao huo utakuwa umefungwa na itakuwa hakuna njia nyengine. 
“Lengo la uwamuzi huo wa Saudi Arabia ni kuwaondoshea mahujaji usumbufu usiowalazima wakati wa kutekeleza ibada hiyo,”alisisitiza Ustaadh Khalid. Amewakumbusha mahujaji watarajiwa kuwa waangalifu na mizigo yao wakati wa safari na wanapokuwa nchini humo na watakaporejea kuchukua kiwango cha mizigo kinachokubalika kwenye ndege. 
Akifungua Kongamano hilo lililoandaliwa na Umoja wa Taasisi za Hijja Zanzibar (UTAHIZA) Mwenyekiti wa Bodi Sheikh Khamis Abdulhamid amewasisitiza waislamu wenye uweze kutekeleza ibada ya hijja ili kukamilisha uislamua wao. 
Mwaka huu Tanzania imepewa nafasi 3,000 kupeleka mahujaji nchini Saudi Arabia ambapo ibada hiyo hutekelezwa kila mwaka mwezi wa mfunguo tatu.
 Ustaadh Seif Shaaban akisoma Qur-an tukufu ikiwa ni ufunguzi wa kongamano lililoandaliwa na Umoja wa Taasisi za Hjja Zanzibar (UTAHIZA) lililowashirikisha mahujaji watarajiwa katika ukumbi  wa Beit al Yamin Malindi Mjini Zanzibar. 
 Katibu wa UTAHIZA Ustaadh Ali Adam akitoa historia ya Umoja huo na kazi zake katika kongamano lililofanyika Malindi Zanzibar.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Umoja wa Taasisi za Hijja Zanzibar  Sheikh Abdulhamid akifungua Kongamano la mahujaji watarajiwa katika ukumbi wa Beit al Yamin Malindi Zanzibar, kulia ni Mwenyekiti wa Umoja huo na kushoto Sheikh Othman Maalim.
 Ustaadh Khalid Mohammed Mrisho akiwasilisha mabadiliko ya taratibu mpya za Ibada ya Hijja katika kongamano la mahujaji watarajiwa lilifanyika Malindi Zanzibar.
 Baadhi ya mahujaji watarajiwa wakimsikiliza Sheikh Othman Maalim alipowasilisha mada ya umuhimu wa kutekeleza ibada ya hija na madhara ya kuchelewesha kutekeleza ibada hiyo katika kongamano liliofanyika Malindi Mjini Zanzibar.
Hujaji mtarajiwa Abass Imtiyaz akiuliza swali katika kongamano lililoandaliwa na Umoja wa Taasisi za Hijja Zanzibar katika ukumbi wa Beit al Yamin Malindi Zanzibar. Picha zote na Makame Mshenga-Maelezo Zanziba.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...