Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza Askofu Mkuu Wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) Dkt.Stephen Munga wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 125 ya dayosisi hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Mbuyukenda mjini Tanga leo. Picha na Freddy Maro.
------------------------------------
Sehemu ya hotuba ya Rais Kikwete juu ya 
Dhima ya Viongozi wa Dini na Uchaguzi Mkuu
 Huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu ambao pia una umuhimu wa aina yake katika historia ya nchi yetu.  Tunaiaga Awamu ya Nne na kuikaribisha Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu. Niruhusuni nitumie fursa hii kuwaomba viongozi wa dini muiombee nchi yetu ipite kipindi hiki kwa salama na amani.  
Uzoefu wa nchi nyingi za Afrika, chaguzi hutoa mwanya kwa uvunjifu wa amani. Haijawa hivyo kwetu, lakini haina maana kuwa tunayo kinga ya milele. Hata na sisi tunaweza kuwa kama wale iwapo yale yaliyowafikisha wenzetu hapo hatutayaepuka.
Mafanikio yetu ya  kuendesha uchaguzi kwa amani na usalama yametokana na tahadhari ambazo Serikali na viongozi wa dini tumekuwa tukizichukua.  Tuendelee kufanya hivyo. Tusiwape mwanya wanasiasa wenye dhamira ovu kuwafarakanisha Watanzania.  
Tuendelee kukemea matumizi mabaya ya fedha,  rushwa, hila, ghilba na hujuma katika chaguzi.  Tunapaswa kufanya hivyo tena zaidi sasa, wakati wa michakato ya ndani ya vyama vya siasa na baadae wakati wa uchaguzi.  
Tuwakemee wanasiasa  wapenda madaraka kwa gharama yoyote, ambao watataka kutumia fedha kununua ushindi au  ubaguzi wa rangi, kabila, dini na kadhalika, kuwabagua wapinzani wao na kujijenga kisiasa.  
Nawaomba msiwasikilize wala kuwaendekeza kwani mchezo wao ni mauti yetu.   Wakatalieni kwa macho makavu na kwa kweli. 
Hatupaswi kukaa kimya dhidi ya watu wanaokiuka maadili na kuchochea mifarakano katika taifa letu. Hawa si watu wema watatufikisha pabaya. Hawaitakii mema nchi yetu.  Kamwe tusiruhusu wachezee dini zetu ambazo ni mhimili muhimu sana wa amani yetu. 
Tofauti na ukabila ambao pamoja na ubaya wake, lakini unaweza kuhusisha eneo dogo, dini unahusisha nchi nzima.  Hakuna mtu, dini wala eneo litakalonusurika. Tutapoteza ile sifa yetu ya kihistoria ya kuwa lulu na mfano wa amani katika Afrika.  
Tusikubali kumchukiza Mungu  akatukasirikia na kutuadhibu kwa jambo ambalo liko ndani ya uwezo wetu kulizuia lisitokee.  Kwa kweli mambo yakiharibika,  hatuwezi kumlaumu mtu mwingine yeyote bali  sisi wenyewe.  Katu hatuwezi kusema ni mapenzi ya Mungu bali itakuwa ni makosa yetu wenyewe.
Nawaomba viongozi wa dini mlisaidie taifa letu.  Limeni mraba wenu vizuri nasi tulime wetu. Msiwape nafasi viongozi wa siasa na hata wa dini kutumia majukwaa ya dini kuendeleza maslahi yao ya kisiasa na  hasa kupandikiza chuki katika jamii.  
Tunawategemea  viongozi wa dini msiwe sehemu ya makundi ya wagombea au vyama vya siasa. Mnatakiwa msiwe na upande bali  muwe juu ya pande zote. Hapo ndipo mtakapofanya vizuri kazi yenu ya ulezi na kuponya  taifa iwapo kutatokea matatizo.
Hatuwategemei viongozi wa dini muwapangie waumini wenu vyama au viongozi wa kuwachagua. Tunawategemea kuwahimiza na kuwakumbusha kuutumia  haki na wajibu wao  vizuri, muwahimize na kuwakumbusha kuwa watatakiwa kufanya mambo matatu muhimu. 
Kwanza, kujiandikisha, pili, kujitokeza kwenda kupiga kura na tatu kuchagua viongozi wazuri, wasiokuwa waovu, wasiofanana na uovu na kuukaribia uovu, watakaosukuma mbele gurudumu la maendeleo na kujali maslahi mapana ya jamii husika na nchi yetu.

Kusoma hotuba yote BOFYA HAPA



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...