Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitaka maelezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo na Mizani, Bibi Magdalena Chuwa (kulia) kuhusu sababu zilizomfanya azuie matumizi ya flow Meter katika kuhakiki kiwango cha mafuta yanayoingia nchini kupitia bandari ya Dar es salaam wakati alipofanya ziara kwenye badari hiyo Februari11, 2016.

SERIKALI imeamua kuwasimamisha kazi watendaji wawili kutoka Wakala wa Vipimo nchini (WMA) kuanzia leo ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa mafuta bandarini kutokana na zuio la kufunga kwa mita kwa zaidi ya miaka mitano.

Waliosimamishwa kazi ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Bi. Magdalena Chuwa na Meneja Vipimo Kitengo cha Bandari, Bi. Bernadina Mwijarubi. Bi. Mwijarubi ndiye anashughulikia kitengo cha mafuta bandarini.

Akitangaza uamuzi huo kwenye kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika leo (Ijumaa, Februari 12, 2016) ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Adelhelm Meru awaandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi huo.

“Katibu Mkuu Viwanda, waandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi. Katika kipindi hiki hawatatakiwa kusafiri kwenda popote hadi uchunguzi utakapokamilika. Pia utafute mtu wa kukaimu nafasi hiyo ili kazi ziendelee,” alisema.

Waziri Mkuu pia amesema ofisi yake itawaandikia barua ofisi ya TAKUKURU na polisi ili wafuatilie suala hilo mara moja na ikithibitika kuwa walihusika hatua rasmi zitachukuliwa na itathibitika hawakuhusika basi watarudishwa.Waziri Mkuu pia aliagiza mfumo wa upimaji mafuta kwa kutumia flow meters uendelee kutumika na ule upimaji wa kukadiria uache kutumiwa mara moja.

Jana (Alhamisi, Februari 11, 2016) Waziri Mkuu alifanya ziara kukagua flow meters za zamani zilizopo Kurasini (Kurasini Oil Jetty) na kisha akatembelea na kukagua flow meters mpya ambazo zinajengwa Kigamboni. Mita hizo zimegharimu dola za marekani milioni 6 (sawa na sh. bilioni 12.96/- za sasa).

Pia Waziri Mkuu alitembelea sehemu ya kuchukulia mafuta yanayotoka bandarini (TPA Manfold) iliyoko Kigamboni na kukagua mitambo ya kusambazia mafuta kwenye matenki ya mafuta ya kampuni ya TIPER yaliyoko Kigamboni yanayomilikiwa kwa ubia baina ya Serikali na kampuni ya Oryx Energies.

Katika ziara hiyo ilibainika kuwa Kampuni ya TIPER imejiunganishia bomba la moja kwa moja kutoka kwenye bomba kubwa la mafuta linalotoka bandarini hali iliyomlazimu Waziri Mkuu kuagiza kwamba bomba hilo litolewe kwenye maungio hayo ndani ya mwezi mmoja.

“Jana niliagiza kuwa bomba hilo ling’olewe. Nimetoa mwezi mmoja ili kurekebisha mfumo huo. Simamieni vizuri na kuhakikisha kuwa na wao pia wanarudi kwenye manfold kama ilivyo kwa wengine,” alisema Waziri Mkuu.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
IJUMAA, FEBRUARI 12, 2016.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Safi sanaa hao ndio mojawapo ya watu walio hiaribu selikari ya kikwete timua wote hao

    ReplyDelete
  2. He he he he, ni pale ambapo Mdhibiti (Inspector) wako anapoamrisha gari lako lisitumike kwa kuwa fundi wako kafunga spare parts fake hivyo usije ukapata ajali alafu wewe unaamua kumsikiliza fundi wako na kumfukuza kazi Mdhibiti wako. Mita ile ilikuwa imeshachezewa na hao hao waliomchongea asimamishwe kazi. Kuifunga ilikuwa sahihi kuhakikisha haitumiki kuhalalisha hali ambayo ni ya wizi ili iwe kama vile ni sahihi. Swali aulizwe TPA, ni kwa nini TPA hawakuitengenezwa Mita hiyo ipasavyo toka Mdhibiti aifungie? Alex Bura mdau dar?

    ReplyDelete
  3. Hatimaye gari imepata dereva! Tanzania sasa tutaendelea, safi sana, hakuna kubweteka bweteka.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...