Hilal Hilal wa kwanza kulia mara baada ya
kushinda medali ya Shaba nchini
Mauritius katika mashindano
ya Cana Kanda ya Nne
Muogeleaji namba mmoja nchini kwa upande wa wanaume, Hilal Hemed Hilal ameiomba serikali kufanya jitihada za kutatua changamoto mbalimbali zinazoukabili mchezo wa kuogelea nchini.

Hilal ambaye  hivi karibuni alishinda medali ya  Shaba katika mashindano ya Cana Kanda ya nne alisema kuwa Tanzania ina waogeleaji wengi wenye vipaji na malengo ya kufanya vyema katika mchezo huo, ila tatizo kubwa ni vifaa ambavyo watatumia kufikia malengo yao.

Alisema kuwa moja ya changamoto kubwa ni bwawa la kuogelea lenye vifaa vya kisasa kwa ajili ya kutimiwa na waogeleaji  wa Tanzania katika mashindano na mazoezi.  Alisema kuwa Tanzania ina mabwawa ya kuogelea ambayo hayana ubora kwa mujibu wa sheria na taratibu za mchezo huo kama za chama cha kuogelea Duniani (Fina) na chama cha Afrika (Cana).

Alifafanua kuwa mabwawa mengi ya Tanzania ni ya mita 25 ambayo hayatumiki katika mashindano ya kimataifa kama ya Cana, Michezo ya Jumuiya ya Madola, Olimpiki na mashindano ya dunia ya kuogelea.

“Mabwawa yapo, lakini si ya viwango vya Cana na Fina, mbali ya mabwawa pia tunahitaji  touchpad  kwa ajili ya kurekodi muda kwa muogeleaji   siyo kwa kutumia stop-watch kama ilivyo sasa, katika mashindano ya kimataifa, stop watch zinatumika sambamba na touchpad ambayo inaendeshwa kisasa si kwa mtu kuendesha kifaa hicho,” alisema  Hilal.

Alisema kuwa mbali ya  mabwawa ya kisasa, mabwawa hayo pia hayana vifaa vinavyotakiwa kutimia wakati wa kuanza kuogelea ‘Diving blocks’ ambazo ni za kielektroniki. Alisema kuwa mara zote wao huvitumia vifaa hivyo wanapokwenda nje ya nchi kwenye mashindano.

“Hapa hakuna jinsi, unalazimika kuwahi siku mbili kabla ili ufanye mazoezi, lakini wenzetu wanavyo katika nchi zao, pia hata vilabu vya mchezo huo wanatumia vifaa hivyo, ni changamoto kwetu kwani unaweza kufutiwa matokeo kwa kushindwa kuanza kwa mujibu wa taratibu,” alisema.

Alisema kuwa pamoja na ukweli kuwa serikali ina majukumu mengi, kwa niaba ya waogeleaji anaomba changamoo hizi zifanyiwe kazi na kuweza kupata hata bwawa moja la kisasa la kuogelea lililosheheni vifaa hivyo vya kisasa.

Aliongeza kuwa mchezo wa kuogelea kwa sasa unashika kasi kubwa, lakini viongozi wa vilabu wanaweza kukata tama kutokana na changamoto hizo.  Hilal pia amewaomba wadau kusaidia serikali kutatua tatizo hili.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...