Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe (pichani) amesema ujangili nchini hufanyika katika ngazi tano ukiwahusisha baadhi ya wananchi wanaoishi kwenye maeneo yanayopakana na hifadhi na watumishi wasio waaminifu.
Ngazi nyingine ni wawindaji haramu wanaojihusisha moja kwa moja na kuua wanyama, wasafirishaji na madalali; wawezeshaji kwenye ngazi ya nchi zinakonunuliwa nyara na wasambaza silaha ambao ni kiungo kati ya majangili nguli na watakatishaji fedha. Ngazi ya mwisho ni majangili nguli wa kimataifa.
Profesa Maghembe ambaye alitaja ngazi hizo jana bungeni alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2016/17, alisema kutokana na hali hiyo, wizara imeimarisha kitengo chake cha intelijensia na kufanya doria kwa kuzingatia mfumo wa makundi hayo.

Alisema kesi 161 zilimalizika kwa wahalifu 53 kuhukumiwa kifungo cha jumla ya miezi 6,360 na Sh363.9 milioni kulipwa kama faini.
“Kati ya wahalifu waliohukumiwa, wanane ni majangili nguli wenye mitandao ya kimataifa,” alisema Profesa Maghembe.
Alisema katika doria zilizofanyika, nyara mbalimbali za Serikali zilikamatwa ambazo ni pamoja na mijusi 315, kobe 202, tumbili 81 na nyani mmoja.
Profesa Maghembe alisema vipande 253 vya meno ghafi ya tembo vyenye uzito wa kilo 634 na vipande 34 vya meno ya tembo yaliyochakatwa vyenye kilo mbili, vilikamatwa.
“Vilevile, kilo 10,096 za nyamapori ya wanyama aina mbalimbali na ngozi 39 za wanyamapori zilikamatwa. Pia, bunduki 85 na risasi 1,235 za aina tofauti zilikamatwa,” alisema.
Majangili watajwe
Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mhe. Catherine Magige alisema haiwezekani Serikali na Bunge wakawa wanapambana na ujangili huku baadhi ya wabunge wakidaiwa kuhusika.
Magige alitaka Bunge lifanye uchunguzi na kujua wabunge majangili ni kina nani ili waweze kutajwa kwa kuwa tembo wanakaribia kuisha nchini.
“Hakuna mbunge ambaye yuko juu ya sheria, hivyo watajwe kwa kuwa haiwezekani tunapambana na ujangili halafu kumbe wengine wapo humuhumu,” alisema Magige.
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa wizara hiyo, Esther Matiko alisema suala la ujangili nchini limekuwa ni tishio kwa wanyama na hata binadamu wanaofanya shughuli ndani ya hifadhi.
“Ujangili nchini umeiletea nchi sifa mbaya kimataifa. Serikali hii yenye falsafa ya kutumbua majipu lazima sasa ijielekeze katika kuwatumbua wale wote wanaohusika katika kukwamisha kesi za ujangili ili zisimalizike kwa wakati,” alisema Matiko.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...