Mkurugenzi wa Idara ya Ajira Ameir Ali Ameir
Na Miza Kona Maelezo- Zanzibar 

Mkurugenzi wa Idara ya Ajira Ameir Ali Ameir amesema tatizo la ajira nchini bado ni changamoto kubwa kwa vijana kutokana vijana wengi kukosa sifa za kuajiriwa na baadhi yao kuchagua kazi za kuajiriwa.

Hayo ameyasema leo katika Ukumbi wa Kidongo chekundu wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya Kuwajengea Uwezo wa Kamati za Ajira za Wilaya za Mjini na Magharibi.

Amesema vijana ndio nguvu kazi katika jamii hivyo wana nafasi kubwa katika kulitumika Taifa kwa kufanya kazi lakini mtazamo wa vijana bado ni tatizo na baadhi wamejenga tabia ya uvivu unaopelekea kuwepo kwa vijana wengi wanaomaliza masomo wakiwa wazururaji wasio na ajira.

Mkurugenzi huyo amezitaka kamati za ajira kujipanga vizuri kuyafuatilia matatizo yanayowakabili vijana kupitia vigezo vyao, masheha, waajiri, mtazamo pamoja Utamaduni wao ili kuwanusuru kujiingiza katika vikundi viovu.

“NI kazi ya kamati kupita kwa waajiri ili kuangalia Changamoto, mafanikio attitude na Utamaduni kwa vijana pia unaweza kufahamu matatizo ya vijana kupitia vigezo vyao pia wazee wana nafasi gani katika kuwasaidia vijana,” alifahamisha Mkurugenzi Ameir.

Aidha amezifahamisha kamati hizo kutafuta taarifa yakinifu kwa vijana ili kupata kujua matatizo ya ajira yanayowakabili na kuweza kuwasaidia na kuwaingiza katika soko la ajira.Ameeleza kuwa vijana wanahaki ya kupata kazi yenye heshima inayoendana na mazingira bora ambayo yatamjenga kuweza kufanya kazi kwa ufanisi na kumpatia kipato cha kujikimu kimaisha na kuondokana na utegemezi.

Akiwasilisha Mada ya Mpango Kazi wa Ajira kwa Vijana Afisa Ajira Kutoka Idara ya Ajira Mustafa Hassan Makame amesema serikali imeweka mikakati mbali mbali ili kuhakikisha inakabiliana na tatizo la ajira na kuona kwanba tatizo hilo linapungua nchini.“Ujasiri amali ni njia ya kutatua tatizo la ajira kwa vijana na sio ajira za serikali peke yake hivyo vijana wana nafasi kubwa ya kujiajiri wenyewe,” ameeleza afisa huyo. 

Nae Mtaalamu kutoka Shirika la Kazi Duniani Edmund Mushy amesema serikali pekee haiwezi kulitatua tatizo la ajira kwa vijana ni lazima pawepo mashirikiano na wadau wengine ikiwemo sekta binafsi na taasisi nyngine kwani nao wana mchango mkubwa katika kukuza ajira nchini.

Wakichangia mada washiriki wa mafunzo hayo wameiomba wizara kuweka mratibu wa ajira katika Wilaya zote atakaeshughulia masuala ya ajira ili kuondosha usumbufu uliopo katika wilaya hizo na kamati ziweze kufanya kazi walizopangiwa kwa ufanisi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 04, 2016

    Elimu yetu pia ibadilike ili ijikite kwenye kuwezesha vijana kujitegemea wanapotoka masomoni badala tu ya kungoja kuajiriwa.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...