THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Gadget

This content isn't available over encrypted connections yet.

MAAFISA 12 WATEULIWA KUWA WAJUMBE WA BARAZA LA KUSIMAMIA MFUMO WA UTOAJI LESENI ZA BIASHARA ZANZIBARA

Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mh. Amina Salum Ali kwa mujibu wa sheria ya kusimamia mfumo wa Utoaji Leseni za Biashara Nam. 13 ya mwaka 2013 amewateua maafisa 12 kuwa wajumbe wa Baraza la kusimamia mfumo wa utoaji leseni za Biashara Zanzibar. 

Uteuzi wa wajumbe wa kusimamia mfumo wa utoaji leseni za Biashara unafuatia uteuzi wa Mwenyekiti wake uliofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Muhamed Shein. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko wajumbe walioteuliwa ni Hussein Migoda Mataka kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Ashura Mrisho Haji kutoka Wizara ya Habari, Utalii Utamaduni na Michezo na Amour Ali Mussa kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za Serikali. 

Wengine ni Hajar Idrisa Haji wa Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Abeida Rashid Abdalla wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu, Rashid Ali Salim Katibu Mtendaji Baraza la Kusimamia Mfumo wa Utoaji Leseni za Biashara na Omar Said Shaaban kutoka Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima (ZNCCIA) 

Wajumbe wengine wa Baraza hilo ni Khamis Salum Ali kutoka ZNCCIA, Mohamed Salim Mohamed wa Jumuiya ya Watembeza Watalii (ZATO), Salmin Sharif Khatib wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, Abdulaziz Hamid Mahmoud na Fatma Mussa Magimbi kutoka sekta binafsi. 

Uteuzi huo umeanza tarehe 24 August 2016. 

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR


MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AHUDHURIA KIKAO CHA SADC TROIKA MJINI MBABANE SWAZILANDMakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia) akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi na Balozi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Innocent Shio (katikati) kulia ni Waziri Mambo ya Njena ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) muda mfupi kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Troika Summit) unaowahusisha Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika umefanyika mchana huu katika ukumbi wa Grand- Lozitha mjini Mbababe Swaziland.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akijianda na mkutano wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Troika Summit) unaowahusisha Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika umefanyika mchana huu katika ukumbi wa Grand- Lozitha mjini Mbababe Swaziland.
Hii ndio muonekano wa Ukumbi wa Mkutano wa Mandvulo Grand uliopo Lozitha mjini Mbabane Swaziland ambapo mkutano wa 36 SADC unafanyika.

.............................................................

Mkutano wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Troika Summit) unaowahusisha Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika umefanyika mchana huu katika ukumbi wa Grand- Lozitha mjini Mbababe Swaziland.

Mkutano huo wa Troika unaohusisha nchi Tatu ambazo ni za Utatu ikiwemo Tanzania, Msumbiji na Afrika Kusini ambapo kwa kuzingatia utaratibu huo mkutano huo unahudhuriwa na Wakuu wa nchi na serikali wa Msumbiji kama Mwenyekiti wa Asasi hiyo (SADC Organ Troika Summit) na Afrika Kusini kama mwenyekiti aliyetoka na Tanzania inatarajiwa kukabidhi uenyekiti wa Asasi hiyo.

Baadhi ya ajenda ambazo viongozi hao watajadili kwenye mkutano huo ni hali ya ulinzi na usalama katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Madagascar na Lesotho, masuala ya upatanishi na utatuzi wa migogoro pamoja na maombi ya Burundi na Comoro kutaka kujiunga katika Jumuiya ya Mandeleo Kusini mwa Afrika- SADC.

Katika mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anawakilishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Ufunguzi rasmi wa mkutano wa SADC utafanyika terehe 30-Aug-16 katika ukumbi wa Grand- Lozitha mjini Mbababe Swaziland ambapo pamoja na Mambo mengine mkutano huo utatoa zawadi kwa wanafunzi walioshinda katika uandishi wa insha katika jumuiya hiyo.


BOFYA HAPA KWA PICHA ZAIDI


MPINGA CUP 2016 YAKONGA NYOYO ZA WAKAZI WA KITUNDA.

 Polisi Konsitebo wa Kikosi cha Usalama Barabarani Makao Makuu, Sharifa Ismaili akikabidhi mipira kwa moja ya timu zilizofanikiwa kuibuka na ushindi kwenye michezo ya MPINGA CUP 2016, makundi raundi ya kwanza kutoka kundi C iliyofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Kitunda, Lengo la Mashindano haya ni kutoa Elimu ya Usalama Barabarani kwa madereva wa Pikipiki ususani waendesha Boda Boda katika mkoa wa Dar es Salaam.
  Staff Sajent wa Polisi, Enock Machunde akifundisha jambo kwa madereva wa Boda boda wakati wa michezo ya Mashindano ya MPINGA CUP 2016 kundi C zilizofanyika kwenye Uwanja wa Kitunda Shule ya Msingi siku za Jumamosi na Jumapili, Lengo la Mashindano haya ni kutoa Elimu ya Usalama Barabarani kwa madereva wa Pikipiki ususani waendesha Boda Boda katika mkoa wa Dar es Salaam.
Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Eric Ndidi akitoa  mipira kwa timu za kundi C zilizofanyika kwenye Uwanja wa Kitunda Shule ya Msingi siku za Jumamosi na Jumapili, Lengo la Mashindano haya ni kutoa Elimu ya Usalama Barabarani kwa madereva wa Pikipiki ususani waendesha Boda Boda katika mkoa wa Dar es Salaam (Picha na Traffic Makao Makuu).Na: Traffic Makao Makuu.
MASHINDANO ya Kombe la MPINGA CUP 2016 hatua ya makundi inayoendelea kwenye Mkoa wa Kipolisi Ilala iliyopangwa kwenye makundi sita tayari makundi matatu yamekamilisha ratiba baada ya kupata washindi wa michezo yao ya awali kutoka kundi C, timu hizo zimechuana kuwania nafasi ya kusonga hatua ya pili baada ya jana kukamilisha ratiba hiyo na kuwa kundi la tatu kuungana na kundi A na B ambayo michezo yake imeshakamilika.

Mchezo wa kwanza wa kundi C ulianza majira ya saa nne asubuhi katika Uwanja wa Kitunda Shule ya Msingi ikiwa ni siku ya Jumamosi tarehe 27/8/2016 ambapo timu ya Chakenge F.C iliweza kucheza dhidi ya timu ya Mara fc ikifuatiwa na Mchezo wa pili ambao timu ya Kivule C.C.M (A) ilipata Ponint za mezani baada ya timu ya Polisi Kitunda kushindwa kutokea Uwanjani na kukabidhiwa Mpira mmoja kwa ajili ya  kujinoa kwa kinyang’anyiro cha mzunguko wa pili.

Mchezo mwingine ilikuwa ni kati ya timu ya Mwembeni Fc Kivule iliyoshindwa kutumia vyema nafasi walizopata kipindi cha kwanza ambapo waliambulia kupata goli 1 dhidi ya wenzao wa Amani fc wakati timu ya Matembele Kivule walishinda kwa kupata magoli mawili (2) katika mchezo wa tatu huku mchezo wan ne (4) Njia Panda Msikitini fc Kitunda ilitolewa kwenye mashindano na timu ya Relini Kitunda iliyoibugiza kwa jumla ya mabao 3-2 na kuzawadiwa mpira ili wakajiweke vema na mzunguko wa pili.

Mwendelezo wa Mashindano haya ya MPINGA CUP 2016, ilifuata siku ya 28/8/2016 Siku ya Jumapili na michezo iliyochezwa ilikuwa ni mitano (5) ikiwa na jumla ya timu kumi zilizokutana kwenye kutafuta nafasi ya kusonga mbele hatua ya kwanza mtoano, Katika Mchezo huo mgumu kwa timu zote mbili, Matembele fc (KIPUNGUNI) dhidi ya timu ya Pentagini Fc ambapo mshindi alikuwa ni Matembele Kipunguni kwa njia ya Penalt -4-3 na kuzawadiwa mpira kwa ajili ya kwenda kujiandaa na mchuano wa dulu la pili.

Mchezo mwingine ulizikutanisha timu za Kitunda fc Kivule iliyocheza na timu ya Mwembeni fc  Kivule na timu ya kitunda Fc ilifanikiwa kuibuka na Ushindi wa mnono wa mabao 3-1 dhidi ya wenzao wa Mwembeni Fc na kuzawadiwa Mpira moja kwa ajili ya kwenda kujiandaa na raundi inayofuata.

Na mchezo wa Tatu uliokuwa na mshikemshike mkubwa dhidi ya timu zote kwa Mashabiki wao, Timu ya MACHIMBO F.C walifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya MUSOMA BUCHA F.C MACHIMBO ambayo hata hivyo mchezo huo ulimalizika kila timu ikiwa na mashike mshike mkubwa na ulikuwa ni mchezo wa kusisimua kutokana na ulivyochezwa kwa ufundi mkubwa na wachezaji wa timu zote mbili hata ivyo mshindi alizawadiwa mpira kwa lengo la kwenda kufanya maandalizi mazuri ya mzunguko wa pili.

Michezo yote hiyo iliongzwa na Mafunzo Muhimu kwa Walimu wa Masuala ya Elimu ya Usalama Barabarani ambao walitoa Mafunzo hayo kwa timu zote kabla ya kuingia uwanjani huku wakifundidishwa pia Alama za Barabarani na Kuulizwa Maswali na Washindi mbali mbali walizawadiwa Furana kutoka kwa wadhamini Mbali Mbali wa Mashindano haya ya MPINGA CUP 2016 yanayofanyika kwenye Mkoa wa Kipolisi ILALA.

Ambapo timu ya Kitunda Sabato Fc ilifanikiwa kuifunga timu ya Kipunguni Relini kwa jumla ya mabao 2-0 katika mchezo ambao ulikuwa wa Upande mmoja huku wachezaji wa timu ya Kipunguni Relini wakisingizia Uwanja kuwa na Michanga wakilinganisha na Beach Soccer, pamoja na yote lakini hatimaye washindi walipatikana na kufnikiwa kijipatia zawadi ya mpira mmoja kila timu iliyoibuka Kidedea.

Mchezo wa Mwisho Timu ya Kivule Silali ilipepetana na timu ya Nyantila fc, timu mbili ambazo ni wapinzani wa jadi walijikuta wakimaliza dakika 90 kwa kutoshana nguvu baada ya kumaliza wakiwa wamefungana bao moja kwa moja 1-1. Lakini hata hivyo kutokana na Sheria ya Mashindano mshindi ni lazima apatikane, walikwenda kwenye mikwaju ya Penalti na mshindi kuwa timu ya Nyantila Fc waliopata mikwaju ya Penali nne (4) huku wenzao wa timu ya Kivule Silali wakiambulia kupata mikwaju miwili (2) ya Penalti na hivyo kumaliza Kundi hilo na Sasa Mashindano Haya ya MPINGA CUP 2016 yatafanyika Kiwalani wiki hii kama ratiba inavyoonyesha.

RATIBA YA MASHINDANO YA BODABODA KUNDI D:

Uwanja ni Chuo cha Walemavu Kiwalani Tarehe 3/9/2016.

1. Mafundi Fc Vs PANDA KIWALANI F.C

2. BOMBOM F.C vs KIJIWE SAMLI KIWALANI
3. YOMBO HOSPT.KIWALANI vs MORNING STAR KIWALANI
4. KIPAWA FC vs KIPAWA SHELI FC
5. VINGUNGUTI SCANIA vs KIZOTA F.C VINGUNGUTI
6. MORNING STAR F.C vs WASHAWASHA F.C
7. KIWALANI BEACH F.C vs BODABODA GARDEN

KAtika UWanja huo huo tarehe 4/9/2016
1. VINGUNGUTI RELINI vs MAZIZI F.C

2. MTI PESA vs MASHUJAA F.C
3. TABATA DARAJANI F.C vs BALAKUDA HIGHLAND FC
4. GOGOVIVU F.C vs BODABODA F.C
5. MANDEZE F.C vs YOMBORELI F.C
6. VIPAJI FC vs GOLAN F.C

Inavyoonekana kwenye kundi hili kutakuwa na ushindani mkubwa sana kutokana na timu nyingi kujitokeza kujiandikisha kutoka maeneo ya kundi D, ambapo jumla ya 14 zitacheza siku hiyo ya jumamosi na siku inayofuata jumla ya timu 12 zitacheza na kupata washindi pekee watakaosonga mbele hatua inayofuata ya mashindano haya a kusisimua na yenye mafunzo mazuri kwa madereva wa Boda boda.

Wadhamini mbali mbali wamejitokeza kudhamini na kuweza kufanikisha michezo hii kuwa ya aina yake mwaka huu ikiwa ni pamoja na Udhamini Wa G.S.M wauzaji wa Piki waliotoa zawadi ya Pikipiki kwa Mshindi, Cool Blue Tanzania ambao kwa hakika wameonyesha Sapoti nzuri kwa kutuhakikishia Maji kwa wachezaji wakati wote wa michezo sambamba na kampuni ya Coca Cola,Big Bon, NMB, Zantel, Haki Elimu, Star Times, Windhoek, Red Bull, NHIF, PUMA, Yono, Dar City Promotions, TBL, Milcom, E.F.M Radio, T-Marc Tanzania, Michuzi Blogs, Mwananchi Communications, Dira Tv, My Way Entertainment, Mashujaa Band, MpaluleBlogs: Miss Demokrasia Tanzania, Balozi wa Demokrasia Tanzania, na Jeshi la Polisi Tanzania.


Kampuni ya TTCL kusaidia mchezo wa riadha nchini.


Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Nicodemas Mushi (kushoto) akimkabidhi tuzo kwa niamba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye (kulia) iliyotolewa na TTCL kwa mwanariadha, Alphonce Simbu aliyefanya vizuri katika mashindano ya Olimpiki 2016 yaliofanyika jijini Rio De Jeneiro nchini Brazil hivi karibuni. Wengine wanaoshuhudia ni baadhi ya viongozi wa vyama vya riadha Tanzania.
Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Nicodemas Mushi (kulia) akimkabidhi tuzo mwanariadha, Alphonce Simbu aliyefanya vizuri katika mashindano ya Olimpiki 2016 yaliofanyika jijini Rio De Jeneiro nchini Brazil kwa niamba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL. Wanaoshuhudia katikati ni baadhi ya wanariadha waliyoiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo. 
Kushoto ni wachezaji wa timu ya Taifa Tanzania walioshiriki katika mashindano ya Olimpiki ya mwaka 2016 yaliofanyika hivi karibuni jijini Rio De Jeneiro nchini Brazil wakirejesha bendera ya taifa kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye (wa tatu kulia) kwenye hafla ya chakula cha jioni kuwapongeza wachezaji iliyofanyika jijini Dar es Salaam. 
Baadhi ya maofisa wawakilishi wa TTCL wakipiga picha ya pamoja na timu ya riadha iliyoiwakilisha Tanzania mashindano ya Olimpiki 2016 Rio, nchini Brazil.

KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) inafanya mazungumzo na vyama vya mchezo wa riadhaa nchini pamoja na wachezaji wa mchezo huo ili kuandaa mpango utakaowawezesha wanaridha kufanya mazoezi ya kutosha na hatimaye kufanya vizuri katika mashindano yao mbalimbali. Kauli hiyo imetolewa jana na Meneja Uhusiano wa TTCL, Nicodemas Mushi kwa niamba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo alipokuwa akitoa tuzo kwa mmoja wa wanariadha, Alphonce Simbu aliyefanya vizuri katika mashindano ya Olimpiki 2016 yaliofanyika jijini Rio De Jeneiro nchini Brazil hivi karibuni. Mwanariadha Simbu alishika nafasi ya tano katika mbio za marathoni na kuvunja rekodi kwa wanariadha wa Tanzania. 


Kampuni ya TTCL mbali ya kutoa tuzo na fedha zitakazomsaidia mchezaji huyo akiwa mazoezini kwa sasa, imetoa fedha kidogo kwa washiriki wote wa mchezo huo ikiwa ni ishara ya kuwapongeza na kuwatia moyo kutokata tamaa ili waweze kufanya vizuri zaidi katika mashindano mengine yajayo. "...Kwa niaba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk. Kamugisha Kazaura TTCL tumejiunga na wadau wengine wa michezo katika kuwapongeza wanamichezo wa timu ya Taifa ya Tanzania walioshiriki mashindano ya Olimpiki 2016 yaliofanyika jijini Rio De Jeneiro nchini Brazil, TTCL kwa nafasi yetu tumejiweka mstari wa mbele katika kuwasaidia wanamichezo wa riadha, tumejitolea kufanikisha timu ya riadha katika kukaa vizuri kimichezo..," alisema Mushi. 

"...Katika kipindi hiki cha michezo 2016 tumejitolea kuifanikisha timu ya riadha kuweza kushiriki vizuri katika programu za mazoezi, leo wakati wanarejea tumewaunga mkono kwa kutoa tuzo na fedha kwa msindi aliyefanya vizuri mwaka huu na pia kutoa fedha kwa wanamichezo wetu zitakazo wawezesha kufanya vizuri katika mazoezi yao, huu ni mwanzo lengo letu ni kwamba tutaweka utaratibu mzuri wa kuzungumza na vyama pamoja na taasisi zinazosimamia michezo hii ili kuona tunatengeneza utaratibu mzuri zaidi ambao ni endelevu utakaosaidia kukua kwa mchezo huu," 

alisisitiza meneja uhusiano huyo. Tuzo ya TTCL kwa Alphonce Simbu na fedha kwa wanariadha hao zilikabidhiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ambapo aliwapongeza wanamichezo wote wa timu ya tanzania iliyokwenda nchini Brazil kwenye mashindano ya Olimpiki 2016 kwa uzalendo waliouonesha kwa taifa licha ya changamoto anuai. Waziri Nnauye aliwaomba Watanzania kutowakejeli wanamichezo hao kwa maneno ya kuwakatisha tamaa na badala yake kuungana kuwapongeza na pia kutoa ushauri kwa wadau wa michezo ili Tanzania iweze kufanya vizuri katika mashindano yajayo, ikiwa ni pamoja na vyama vya michezo kusaidia kyuongeza idadi ya wachezaji wa timu ya Tanzania. 

Kampuni ya Multichoice Tanzania pia iliungana na TTCL na kuwazawadia ving'amuzi vya DSTV vilivyolipiwa kwa muda wa miezi sita wanamichezo wote wa timu ya Tanzania iliyoshiriki katika mashindano ya Olimpiki mwaka 2016, pamoja na kumsaidia kumuwezesha mwanariadhaa Simbu programu za mazoezi kwa muda wa mwaka mmoja akiwa kama balozi wa kampuni hiyo. Timu ya Taifa ya Tanzania iliyoshiriki katika mashindano ya Olimpiki mwaka 2016 ilikuwa na wanamichezo saba, ambapo wanamichezo wanne walishiriki riadha, wawili waogeleaji na mmoja alishiriki mchezo wa judo.


PROF WANGWE ATAKA WATANZANIA KUENDELEA KUMUUNGA MKONO RAIS MAGUFULI.

Na Daudi Manongi, MAELEZO.
MWENYEKITI wa Bodi ya Wadhamini wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii Prof Samwel Mwita Wangwe amesema kuwa uongozi wa Awamu ya Tano umefanya kazi kubwa katika kuweka maslahi ya Taifa mbele ikiwamo kuongezeka kwa bajeti ya maendeleo na kupunguza matumizi ya serikali.

Hatua hii imesaidia nchi kusonga mbele kupitia uboreshaji wa  utendaji kwa watumishi wa umma na hivyo kujenga imani kubwa kwa wananchi juu ya Serikali yao.

Profesa Wangwe ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es salaam wakati akitoa tathmini ya uongozi wa Awamu ya Tano.

Amesema kuwa Rais Magufuli katika uongozi wake umesaidia  kuokoa fedha nyingi za walipa kodi ambazo zilikuwa zikiishia mikononi mwa watu wachache na kuzielekeza katika shughuli nyingine za maendeleo.

Profesa Wangwe amewataka wananachi kumuunga mkono Rais Magufuli kwenye harakati zake za kupambana na matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kuwa matokeo yake yatasaidia kuijenga Tanzania mpya ambayo kila mwananchi atapata fursa kunufaika na rasilimali za nchi.

“Kwa kweli Rais huyu amefanya mabadiliko makubwa sana na kwa sasa  nchi imerudi katika hali  nzuri,  kwani nchi ilikuwa imefika mahali pabaya na kwa hiyo aliona ni budi kuhakikisha Rushwa na Ufisadi vinakomeshwa na kwa hili ameanza vizuri na nchi inakwenda katika mwongozo mzuri kwani ameboresha utendaji kazini serikalini na kubana matumizi ambayo yamesaidia kuokoa pesa nyingi ambayo inatumika katika maendeleo ya nchi hii”aliongeza Profesa Wangwe.

Mbali na hayo Profesa Wangwe ameshauri Serikali kuweka mfumo mzuri katika ukusanyaji kodi kwa kurasimisha biashara ili mfumo huu wa  EFD utumike kirahisi na pia kutengenezwe mazingira mazuri ya biashara kwa kuweka mazingira rahisi ya kuandikisha biashara kwani huchukua muda mrefu kwani kwa kufanya hivyo kasi ya kurahisisha  utendaji na wafanyabiashara watalipa kodi kwa wingi na uchumi utakua.

Pia Profesa Wangwe ametoa ushauri kwa vyama vya upinzani kuacha na na maandamano yasiyo na tija na badala yake wakae chini na kuzungumza na serikali ilikupata mwafaka na hivyo amani iendelee kuchanua katika nchi hii.


Vyombo vya usimamizi wa Sheria vyatakiwa kutoa adhabu mbadala kwa wahanga wa dawa za kulevya nchini.

Na Eliphace Marwa-MAELEZO

MWENYEKITI wa Bodi ya Taifa ya Misamaha kwa Wafungwa (Parole) Dkt. Augustine Mrema amevitaka vyombo vya usimamizi wa sheria nchini kutoa adhabu mbadala ya kifungo cha nje kwa wahanga wa matumizi ya dawa za kulevya nchini. 

Hatua hiyo inaeelezwa itawezesha kuwapatia huduma bora za matibabu ambazo ni ngumu kuzipata pindi wawapo mahabusu au wakitumikia kifungo katika magereza.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) alisema katika siku za hivi karibuni kumezuga tabia kwa baadhi ya askari polisi kuwageuza mtaji wahanga wa madawa ya kulevya.

“Natoa wito kwa Jeshi la Polisi kuacha mara moja tabia ya kuwabambikia kesi wahanga hawa na badala yake washughulike na wakubwa wa wauza madawa hayo ambao wapo katika jamii na wanafahamika na hata baadhi ya Polisi” alisema Dkt. Mrema

Aidha Mrema alisema idadi ya watumiaji wa madawa ya kulevya imekuwa ikiongezeka kila kukicha nchini hatua inayoisababisha Serikali kuwa mzigo mkubwa katika kuwahudumia ikilinganisha na mahitaji yaliyopo.

Katika barua yake aliyoiwasilisha kwa Rais, Dkt Mrema alisema wahanga hao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa vituo vya tiba, kutengwa na kukamatwa mara kwa mara na polisi.

Kwa mujibu wa Mrema alisema ndani ya barua hiyo pia amemshauri Rais John Magufuli kuwasaidia wahanga hao kupata maeneo maalum ya mashamba kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo ili makundi hayo yaweze kujiongezea kipato.

Dkt Mrema pia aliishauri Serikali kuwapa wahanga hao jukumu la kusafisha Jiji la Dar es Salaam na kuwa walinzi wa wachafuzi wa mazingira. Faini iliyopangwa na jiji ni Tsh. 50,000, kati ya hizo nashauri tsh 20,000 wapewe wahanga hawa ili iwe kama motisha kwao” alisema Dkt Mrema.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa magonjwa ya akili kutoka hospitali ya taifa muhimbili, Dkt. Cassian Nyandindi jamii haina budi kubadili mtizamo kuhusu watumiaji wa madawa ya kulevya, kwa kuwa wahanga hao hawakupenda kuwa wategemezi katika matumizi ya madawa hayo.

Dkt. Nyandindi alisema hospitali hiyo kwa kwa sasa imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya kuwahudumia wahanga wa matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo uhaba wa watumishi pamoja na vituo vya kutolea huduma. 

Dkt. Mrema ameeleza kuwa vijana hawa walipokuwa wakituia dawa za kulevya walidhalilika katika jamii na kuonekana kama wanyama na kupelekea hata jamiii kuwatenga kutokana na vitendo vya uhalifu lakini baada ya kuanza matibabu wamebadilika kitabia na hata jamii imeanza kurudisha imani kwao.

Akielezea kero wanazokutana nazo Dkt. Mrema amesema kuwa wahanga wengi wamekuwa wakikamatwa na Polisi kwa kukutwa na kete moja au mbili na kufunguliwa mashtaka mahakamani.“Nimetoa ushauri badala ya kuwapeleka magerezani wasioanza tiba bali wapelekwe hospitalini na waanzishiwe tiba ili kuwarejesha katika utu wao,” alisema Dkt. Mrema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Parole nchini Dkt. Augustine Mrema (katikati) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati alipokutana nao kuwaeleza umuhimu vyombo vya usimamizi wa sheria nchini kutoa adhabu mbadala ya kifungo cha nje kwa wahanga wa matumizi ya dawa za kulevya nchini ikiwa ni sehemu ya barua yake kwa Rais John Magufuli, kulia ni Dkt. Bingwa wa Magonjwa ya Akili toka Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Cassian Nyandindi na kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Bw. Vincent Tiganya.
Mwenyekiti wa Bodi ya Parole nchini Dkt. Augustine Mrema (kulia) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati alipokutana nao mapema hii leo jijini Dar es Salaam na kuwaeleza umuhimu vyombo vya usimamizi wa sheria nchini kutoa adhabu mbadala ya kifungo cha nje kwa wahanga wa matumizi ya dawa za kulevya nchini ikiwa ni sehemu ya barua yake kwa Rais John Magufuli.


YALIOJIRI KATIKA TAMASHA LA MUZIKI MNENE 2016 WA EFM REDIO

Jumamosi ya tarehe  27/8/2016, kituo cha redio cha efm kilisepa na kijiji cha Boko kama ilivyo kauli mbiu yao ya “Tunasepa na kijiji” katika tamasha la mziki mnene lililoanza na jogging, ikifuatiwa na kutafuta vipaji vya wasanii chipukizi wa muziki wa singeli na jioni timu ya efm redio ikachuana vilivyo na timu ya Boko beach veterans katika mchezo wa mpira wa miguu na baadaye kuamia Fyatanga bar ambapo timu nzima ya Efm, Rdjs iliwasha mziki mnene na kuburudisha wasikilizaji wake.
Rdj’s X5 akisababisha katika Bar, usiku wa muziki mnene.
Mashabiki wa efm wakiserebuka na burudani ya muziki kutoka kwa rdj’s.
Mshindi aliyeshida kucheza ki 4G akikabidhiwa zawadi ya simu na tshirt kutoka Vodacom.
Klabu ya efm jogging wakikimbia na wakazi wa Boko.   
Washiriki 10 waliopatikana katika kumpata mkali wa Singeli michano kupitia funga mtaa ya efm redio wakiwa na majaji.


BREAKING: SERIKALI YAVIFUNGIA VITUO VIWILI VYA REDIO LEO JIJINI DAR

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.

WAZIRI wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye amezifungia radio mbili kwa muda usiojulikana kwa makosa ya kuandaa vipindi ambavyo vimerushwa hewani vinavyoashiria uchochezi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Nape amesema kuwa uamuzi wa kuvifungia vituo hivyo umefikiwa baada ya kujirdhisha kuwa kipindi cha Matukio kilichorushwa Agosti 25, 2016 muda wa saa 2 usiku hadi saa 3 na kituo cha utangazji cha Radio 5 pamoja na kipindi cha Morning Magic katika kipengele cha Kupaka Rangi Agosti 17 vilikuwa na maudhui ya uchochezi unaoweza kuleta uvunjifu wa Amani.

Nape amesema kuwa kufuatia hilo amevifungia kwa muda usiojulikana kwani wamekiuka masharti ya kanuni ya 5 (a, b, c na d) , kanuni ya 6 (2a, b na c) na kanuni ya 218 ya huduma za utangazaji ya mwaka 2005.

Wakati vituo hivyo vikifungiwa kwa muda usiojulikana kamati ya maudhui imepewa jukuu la kuviita na kusikiliza kwa kina Zaidi utetezi wao na ni hatua gani zaidi ya kuchukua dhidi yao kwa mujibu wa kanuni ya huduma za utangazaji.

Nape ameendelea kuvitahadhalisha vyombo mbalimbali vya habari kutoshawishika kuvunja sheria na kanuni zinazoongoza tasnia ya habari ili kulinda heshima ya tasnia yetu na wakati huo kuhakikisha nchi inabaki na Amani, Mshikamano na Umoja. 
Waziri wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, wakati akitangaza kuzifungia radio mbili kwa muda usiojulikana kwa makosa ya kuandaa vipindi na kuvirusha hewani ambavyo vinaashiria uchochezi. 

Waziri wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye akitoa  ufafanuzi alipokuwa akijibu maswali mbalimbali ya Wanahabari,wakati alipokuwa akitoa taarifa ya kivifungia vituo viwili vya radio kwa muda usiojulikana kwa makosa ya kuandaa vipindi vyenye maudhui yenye viashiria vya uchochezi.
 Waziri wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye akifafanua jambo kwa waandishi wa habari.Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya jamii.


MJUE KIUNDANI DIKTETA MZALENDO NA MTANASHATI MUAMAR GADDAFI

Imeandikwa na Geofrey Chambua 
Rais wa zamani wa Marekani Ronald Reagan alimwita Gaddafi 'mad dog' yaani 'mbwa kichaa' na Marekani ililipiza kisasi dhidi ya Libya kwa madai ya kuhusika na mashambulio ya anga barani Ulaya kwa kuvamia miji ya Tripoli na Benghazi mwaka 1986.

Baada ya kuuawa kwa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, walibya na dunia kwa ujumla imeingia katika mitizamo tofauti kuhusu kiongozi huyo huku wengine wakikumbuka mafanikio aliyoleta kwa taifa na wengine wakiangalia picha ya pili ya udikteta wake; 

Unajua ni kwanini Walibya na Afrika ilimlilia Gaddafi?
Mzaliwa wa Juni 7, 1942, 'mtoto wa mfugaji, Muammar Mohammed Abu Minyar Gaddafi alijikuta Raisi wa Libya miaka 27 tu baadae kwani mnamo mwaka 1967 aliingia madarakani kwa kumpindua 'King' Iddris akiyaita mapinduzi ya kiutamaduni-Mapinduzi haya yalimpa jina la shujaa mtanashati (Handsome Hero) kwani alifanya mapinduzi bila kumwaga damu
Haya ni baadhi ya mambo ambayo Gaddafi aliyasimamia na kuyatekeleza katika utawala wake wa miaka 42 kwa Libya.

  
1. Chini ya Utawala wake Walibya walineemeka haswaaa kwani licha ya elimu, umeme, afya na mahitaji mengine ya msingi kuwa BURE, Kwa waliokuwa wakitaka kununua magari, Serikali ililipia kwa asilimia 50 ya bei. Bei ya petroli ilikuwa karibu na bure, lita ililipiwa kwa Dola 0.4.....Hii iliwezekana kutokana na kudhibiti mafuta yatumike kwa manufaa ya wananchi wote na wageni wasubiri (MWENYE BOMBA HAKAI FOLENI)

2. Makazi ilikua ni haki ya msingi nchini Libya, Gaddafi aliwahi kusisitiza kwamba wazazi wake hawawezi kupata makazi hadi kila raia apate makazi/nyuma ya kuishi. Baba wa Gaddafi alifariki dunia wakati yeye na mama yake wakiwa wanaishi katika hema (kijijini kwao).

3. Wanandoa wote wapya nchini humo walipata Dola 50,000 (zaidi ya milioni 100 za madafu) toka Serikalini kwa ajili ya kununua makazi yao kuwasaidia kuanzisha familia mpya na Kila mwanamke aliyejifungua alipata posho ya Dola 5000 (zaidi ya milioni 10 za madafu)
4. Alifanikiwa pia kufuta UJINGA miongoni mwa Walibya (asilimia 25 wa Walibya, wana shahada ya chuo kikuu). Wakati Gaddafi anachukua nchi asilimia ya waliokuwa na elimu ilikuwa 25, kwa sasa inafikia 83 na huenda ANGEUFUTA KABISAA UJINGA kwa njozi zake. Iwapo kuna waliokuwa hawawezi kupata huduma za elimu na afya wanazostahili, Serikali iliwalipia kwa ajili ya kuzipata nje ya nchi, hizi hazikuwa bure, walitakiwa kuchangia, walipata Dola2,300 kwa mwezi kwa ajili ya makazi na usafiri. Kwa waliomaliza vyuo, Serikali iliwapatia posho sawa na mshahara wa maofisa hadi watakapopata ajira yenye uhakika.

5. Kwa waliotaka kuwa wakulima, walipewa ardhi bure, nyumba katika shamba lao, vifaa, mbegu na mifugo kwa ajili ya kuanzisha miradi,

6. Kama hiyo haitoshi, alisimamia mradi mkubwa kabisa wa umwagiliaji, uliopewa jina la Great Man-made River, kuhakikisha maji yanakuwepo kwenye maeneo yote ya nchi yenye jangwa.

7. Wakati wa vikwazo kwa Serikali yake miaka ya 1980, Libya ilikuwa miongoni mwa nchi tajiri kabisa kwa msingi wa pato la ndani, ikiwa na kiwango cha juu cha maisha kuliko Japan. Ilikuwa ni nchi tajiri kuliko zote kabla ya vuguvugu la mapinduzi.

8. Huyu alikua mzalendo wa kweli mwenye njozi za kuikomboa Afrika nzima na kwa kuanzia alianza kushona vazi lenye PICHA ZA VIONGOZI NGULI AFRIKA akiwemo Mwalimu JK Nyerere.

9. Kuhusu mchango wa Gaddafi katika kuziondoa Serikali zote dhalimu Afrika na duniani kwa ujumla, alikuwa na chombo kinachoitwa Revolutionary Council Movement (RCM).Hii ni Kamati ya Vuguvugu la Mapinduzi. Gaddafi alijiona anao wajibu wa kusaidia vuguvugu la mapinduzi ili kusimika mataifa ambayo yatakuwa huru dhidi ya mataifa ya magharibi, Ulaya na Marekani. Kiongozi wake mkuu wa tawi la RCM-Tanzania, alikuwa Aman Nzugile Jidulamabambasi (marehemu).
10. Mwalimu aliwahi kumwambia Gaddafi kwamba pale kwake Butiama, anazungukwa na ndugu zake waislamu lakini hawana mahali pazuri pa kufanyia ibada, Gaddafi akajenga msikiti wa Butiama kulingana na idadi ya waumini wa kijiji cha Butiama. Baadaye Mwalimu akamwambia tena Gaddafi kwamba makao makuu ya chama chake na Serikali yake, Dodoma, hawana msikiti wenye hadhi ya makao makuu ya nchi. Gaddafi akajenga msikiti mkuu wa Dodoma.

11. Benki ya Afrika (BOA) na Kituo cha Redio na Televisheni cha Sauti ya Afrika (Voice of Afrika-VOA), vilianzishwa na utawala wa Gaddafi kutokana na ushauri huo wa Mwalimu. VOA ina idhaa ya Kiswahili, na watangazaji wa idhaa hiyo ni Watanzania na wachache kutoka Kenya.

​12. Gaddafi aliwaamini sana wanawake katika uongozi wake. alibaini kuwa wanawake wana jukumu kubwa zaidi ya kutunza nyumba na watoto. Imani yake (Gaddafi) inasemekana ni kuamini kuwa wanawake wangeweweza kuwa walinzi wake kwani isingekuwa rahisi kwa mwanaume wa Kiarabu kumpiga risasi na kumuua mwanamke. Wengine wamekuwa wakidai kuwa mapenzi ya Gaddafi kuwa karibu na wanawake warembo ndiyo yaliyomfanya aamini katika ulinzi ule wa Amazon Guards.​
Rais Barack Obama wa Marekani amewahi kusema: "Kosa baya zaidi katika urais wangu ni kukosa mpango wowote kwa ajili ya zama za baada ya kumuangusha Muammar Gaddafi nchini Libya."

Kwa mujibu wa kanali ya CNN, Barack Obama ametoa kauli hiyo katika mahojiano na Fox News akijibu swali kuhusu kosa kubwa alilowahi kufanya katika kipindi chake cha urais. Ingawa rais wa Marekani ametetea uingiliaji wa mgogoro wa Libya, lakini ameitaja hali ya hivi sasa nchini humo kuwa ni 'fedheha'. (http://kiswahili.irib.ir/uchambuzi/item/56302-)
Wosia wa Gaddafi kabla ya kifo 

KANALI Muammar Gaddafi, Mfalme wa Wafalme wa Afrika na mtu aliyekuwa na ndoto za kuliunganisha Bara la Afrika, sasa ameyeyuka katika ulimwengu huu, kama mshumaa uliowaka na kuteketea.

HUKU LICHA YA KUKUTWA KWENYE MTARO WA MAJI MACHAFU KABLA YA UMAUTI NA LICHA YA UTAJIRI LUKUKI ALIOKUWA NAO​,​ ALIKUFA AKIMUAMINI MUNGU

Katika sehemu ya wosia wake aliandika maneno haya

........ninaapa kwamba hakuna Mungu mwingine zaidi ya Allah na Muhammad ni Mtume wake, amani iko kwake. Ninaahidi nitakufa nikiwa Muislamu..............

Kanali Gaddafi pia aliwaasa wafuasi wanaomuunga mkono kuendelea kupambana. Alielezea msimamo wake kuwa amechagua kupambana hadi hatua ya mwisho na kufia katika ardhi ya Libya kuliko kuchagua njia nyepesi, ambayo kwa mtizamo wake, ni kitendo cha kujidhalilisha kisichokuwa na heshima, kukimbilia uhamishoni nje ya nchi yake, ambapo tayari alishapata ahadi nyingi za ulinzi.

�Iwapo nitauawa, nitapenda kuzikwa kwa mujibu wa taratibu za kiislamu, nikiwa nimevaa mavazi nitakayokuwa nimevaa wakati kifo changu kikitokea, bila mwili wangu kuoshwa, katika makaburi ya Sirte, jirani na familia na jamaa zangu. 

Wapi walipo The Amazon Guard??.....Itaendelea............


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Bw. Andrew Wilson Massawe akabidhiwa ofisi na Dr. Modestus Kipilimba

Aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa na ambaye sasa ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa Dr. Modestus Kipilimba leo amekabidhi rasmi ofisi kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu mpya Bw. Andrew Wilson Massawe; aliyeteuliwa hivi karibu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu NIDA. 
Katika Hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika Makao Makuu ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA, Dr. Modestus Kipilimba amekabidhi ripoti yenye mjumuisho wa taarifa ya utekelezaji mradi wa Vitambulisho vya Taifa na hatua za utekelezaji. 
Halfa hiyo ilifuatiwa na ziara fupi ya kutembelea kituo cha uchakataji taarifa na uzalishaji vitambulisho (Data Centre) ambapo mbali na kukagua shughuli za uzalishaji, Bw. Massawe alipata fursa ya kukagua mitambo na ubora wa vitambulisho vinavyozalishwa.
 Dr. Modestus Kipilimba (Kushoto) akimkabidhi ripoti ya utekelezaji mradi wa vitambulisho vya Taifa Bw. Andrew Wilson Massawe aliyeteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu NIDA wakati wa hafla ya Makabidhiano katika ofisi za  Makao makuu ya NIDA jijini Dar es salaam.
 Kaimu Mkurugenzi Mkuu NIDA, Bw. Andrew Wilson Massawe akizungumza na wajumbe wa Menejimenti ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa mara baada ya hafla ya makabidhiano

 Kaimu Mkurugenzi Mkuu NIDA, Bw. Andrew Wilson Massawe akikagua mitambo ya uzalishaji vitambulisho alipotembea kituo cha uchakataji na uzalishaji vitambulisho mara baada ya halfa ya makabidhiano. Kulia ni   Dr. Modestus Kipilimba

 Kaimu Mkurugenzi Mkuu NIDA, akikagua mfumo wa uhifadhi taarifa wakati alipotembelea kituo cha uchakataji taarifa (Data Centre) na kushuhudia mfumo wa kielektroniki unavyoendesha shughuli mbalimbali za uzalishaji na uhifadhi wa taarifa katika kituo hicho
 Dr. Modestus Kipilimba (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA Bw. Andrew Wilson Massawe wakiwa katika  picha ya pamoja na Menejimenti ya NIDA, baada ya hafla fupi ya makabidhiano


Kipa Said Kipao wa JKT Ruvu aitwa timu ya Taifa

KOCHA  Mkuu wa timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ‘Taifa Stars’, Charles Boniface Mkwasa, amefanya mabadiliko kwenye kikosi kinachotarajiwa kusafiri Jumatano Agosti 31, 2016 kwenda nchini Nigeria kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2017) dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo, The Super Eagles.

Mabadiliko yaliyofanyika ni kwa kumchukua Kipa kinda wa JKT Ruvu, Said Kipao ambaye anachukua nafasi ya Deogratius Munishi ambaye amepatwa na mshibwa wa kufiwa na baba yake mzazi jana Agosti 28, 2016, jijini Dar es salaam.

Licha ya mchezo huo wa Septemba 3, 2016 kuwa sehemu ya mchuano wa kuwania nafasi ya kucheza fainali hizo za AFCON 2017 huko Gabon, lakini utakuwa ni wa kukamilisha ratiba baada ya Misri kufuzu kutoka kundi G ambalo mbali ya Nigeria na Tanzania, pia ilikuwako Chad ambayo ilijitoa katikati ya mashindano.

Timu hiyo itaondoka asubuhi ya Agosti 31 kuelekea nchini Nigeria huku mchezaji Mbwana Samata akitarajiwa kujiunga na wenzake huko.


NSSF YAMUUNGA MKONO RAIS DK. JOHN POMBE MAGUFULI KWA MKOPO WA SH.BILIONI NNE KWA KIWANDA CHA VIUADUDU KIBAHA.

Na Chalila Kibuda, Globu ya jamii.
SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limetoa mkopo wa dola za Kimarekani  mil. 2.1 (zaidi ya sh bilioni nne) kwa kiwanda  cha kuzalisha  viuadudu vya kuua viluwiluwi vya mbu cha Tanzania Biotech Product  Ltd kilichopo wilayani Kibaha, mkoani Pwani ili kukiongezea uzalishaji wake, hatua inayotajwa kuwa ni kuitikia wito wa Rais Dr John Magufuli wa kuifanyaTanzania kuwa nchi ya viwanda.

Mbali na mkopo huo unaotolewa kupitia benki ya Azania itayayosimamia urejeshwaji wake, pia shirika hilo lipo kwenye mchakato wa kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda vipya na vikubwa zaidi vya kutengezeza nguo, matairi pamoja na sukari hapa nchini.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama mbali na kulipongeza shirika hilo kwa kuunga mkono nia ya Rais na serikali kwa ujumla katika kuelekea uchumi wa viwanda, alisema uwezeshaji wa kiwanda hicho  umeongeza kasi ya vita dhidi ya ugonjwa wa Malaria kwa asilimia tisini (90).

“Kiwanda kipekee barani Afrika na ufanisi wake utawanufaisha si tu watanzania bali Waafrika kwa ujumla na kutuletea fedha za kigeni,  na kuweza kufikia uchumi wa kati katika sekta ya viwanda’’ alisema.

Amesema uamuzi wa shirika hilo kutoa mkopo huo kupitia benki ya Azania utaliwezesha shirika hilo kuwa na msimamizi thabiti wa marejesho ya pesa za wanachama wa mfuko huo.

“Mwanzo kabisa kwenye uamuzi huu  niliomba kupata uhakika fedha za wanachama na nilipohakikishiwa kuwa kuna benki itasimamia mkopo huu basi nikajua pesa za wanachama zipo salama. Niendelee tena kuwaomba wahusika wote wawe makini kwenye pesa hizi,’’ alisisitiza.

Alitoa wito kwa mifuko ya hifadhi hapa nchini kuhakikisha inawekeza zaidi kwenye viwanda huku akiwataka viongozi wa mashirika mbalimbali kuhakikisha wanalinda haki na maslahi ya wafanyakazi wao likiwemo suala la kuwaunganisha wafanyakazi wao na  mifuko ya hifadhi ya jamii.

Akizungumza wilayani Kibaha  wakati wa hafla fupi ya kukabidhi mkopo huo kwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) linalomiliki kiwanda hicho, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof Godius Kahyarara alisema shirika lake lina dhamira ya dhati katika kuwekeza kwenye viwanda nchini ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Tanzania.

“Pamoja na kuitikia wito wa Rais Dk.John Magufuli katika kuibadilisha Tanzania kuwa nchi ya viwanda ili kuiongeza ajira hapa nchini lakini pia tunatarajia kupata faida kupitia marejesho ya pesa hizi,’’ Alibainisha.

Akiwatoa hofu wanachama wa mfuko huo na watanzania kwa ujumla kuhusu usalama wa pesa zao, Prof Kahyarara alisema uamuzi wa shirika kuwekeza kwenye viwanda sio mgeni kwa kuwa ulianza miaka ya nyuma ambapo shirika hilo liliwezesha viwanda vya saruji Mbeya, Mkonge Tanga, Sukari Kagera na kiwanda cha nguo 21st Century cha Morogoro.

“Uwekezaji huo ulionyesha mafanikio makubwa kwa wananchi wengi walipata ajira na shirika lilipata faida iliyokusudiwa na kuboresha mafao ya wananchama.  Tupo makini na aina za uwekezaji na miongoni mwa kanuni tunazotumia katika uwezaji ni suala la tija, faida, usalama na malengo ya mradi husika hususani katika kuinua uchumi wa nchi kwa ujumla,’’ alisema.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya NDC Dkt Samuel Nyantahe alisema mkopo huo utakiwezesha kiwanda hicho ambacho kimejengwa kwa kushirikiana na kampuni ya LABIOFAM SA ya nchini Cuba kupanua uzalishaji wake na kuwa katika nafasi ya kutafuta soko hadi nje ya nchi.

Naye Mkurugenzi wa huduma za sheria wa Benki ya Azania, Bw Geofrey Dimoso alisema benki yake imejipanga kuhakikisha inasimamia urejeshwaji wa pesa hizo kwa mfuko wa NSSF huku akiwatoa hofu wanachama wa mfuko huo kuwa pesa zao zipo salama.
 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya jamii (NSSF)Prof Godius Kahyarara (kulia) akikabidhi mfano wa hundi ya pesa yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 2 na laki 1 (zaidi ya Tsh bilioni nne) kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC)  Dkt Samuel Nyantahe (wa tatu kushoto) ikiwa ni mkopo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji kwenye kiwanda  cha kuzalisha  viuadudu vya kuua viluwiluwi vya mbu cha Tanzania Biotech Product  Ltd kilichopo wilayani Kibaha, mkoani Pwani wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika mwishoni mwa wiki. Wanaoshuhudia ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (katikati), Mkuu wa wilaya ya Kibaha, Bi Assumpta Mshana, (wa pili kulia) Mkurugenzi wa huduma za sheria wa Benki ya Azania, Bw Geofrey Dimoso (wa pili kushoto) na Kaimu Meneja Mkuu wa kiwanda hicho Bw Samwel Mziray.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama Mkuu wa wilaya ya Kibaha, Bi Assumpta Mshana pamoja na  jopo la maofisa  kutoka NSSF, NDC, benki ya Azania na uongozi wa kiwanda cha kuzalisha  viuadudu vya kuua viluwiluwi vya mbu cha Tanzania Biotech Product kwa pamoja wakimsiliza mmoja wa wataalam kutoka kiwanda hicho aliekuwa akifafanua moja ya shughuli za kiwanda hicho.
  Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (kulia) akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya jamii (NSSF)Prof Godius Kahyarara (kushoto) pamoja na viongozi wa NSSF kwenye ziara hiyo.


YANGA YAENDELEA KUHIFADHI VIPORO, MECHI YAO NA JKT RUVU YAPIGWA KALENDA

Na Zainab Nyamka,Globu ya Jamii.
BODI ya Ligi Kuu (TPLB) ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imethibitisha kuwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Young Africans ya Dar es Salaam na JKT Ruvu ya Pwani, uliopangwa kufanyika Jumatano Agosti 31 mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam imeahirishwa mpaka itakapopangiwa tarehe nyingine.

Mabadiliko hayo hayatavuruga ratiba ya mechi zinazofuata za Ligi Kuu ya Vodacom kwa timu husika.

Taarifa hiyo imekuja baada ya uongozi wa Yanga kutuma barua ya kuomba kusogezwa mbele kutokana na idadi kubwa ya wachezaji wake kujiunga na timu zao za taifa na tayari Yanga na JKT Ruvu wameshapatiwa barua za kujulishwa.

TFF imesogeza mbele mchezo huo, na utapangwa tena lini utachezwa, ligi itaendelea Septemba tatu mwaka huu kwa michezo minne kupigwa kwenye viwanja tofauti.

Mbao FC  wataikaribisha Mbeya City katika Uwanja wa CCM Kirumba, Kagera Sugar watakuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Kaitaba kuialika Mwadui FC, Majimaji FC watawakaribisha Mtibwa Sugar kwenye dimba la Majimaji Songea huku JKT Ruvu wakiumana na African Lyon katika uwanja wa Mlandizi.


WAZIRI MKUU, MAJALIWA AKIWA KWENYE ZIARA NAIROBI.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Rais na Ofisa mtendaji Mkuu wa kampuni ya Sumitomo Corporation ya Japan, Bw. Kunihuru Nakamura  katika Mkutano wa TICAD 6 uliofanyika Nairobi Kenya, Agosti 28, 2016.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Rais na Ofisa mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Sumimoto Corporation ya Japan katika mkutano wa TICAD 6 uliofanyika jijini Nairobi Agosti 28,2016.
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Sumimoto ya Japan, Bw. Kanihuru Nakamura  (kushoto kwake) baada ya mazungumzo yao jijini Nairobi Agosti 28, 2016. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa James Mdoe na Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dkt.Adelhelm Meru.  Wanne kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mathias Chikawe.
 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
KWA PICHA ZAIDI BOFYA HAPA.

WAZIRI MKUU AKARIBISHA WAWEKEZAJI KUTOKA JAPAN .
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji kutoka Japan na kusema kwamba kufanyika kwa Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Bara la Afrika (TICAD VI) jijini Nairobi kumetoa fursa kwa Tanzania na nchi nyingine kukutana na wafanyabiashara wakubwa wenye nia ya kuwekeza barani humo.

Ametoa kauli hiyo jana (Jumapili, Agosti 28, 2016) alipokutana faragha kwa nyakati tofauti na viongozi wa makampuni makubwa ya Japan ambao walikuwa wakihudhuria mkutano huo uliofanyika katika kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Jomo Kenyatta (JICC) jijini Nairobi, Kenya.

Mkutano wa sita wa TICAD ambao umemalizika jana, ulilenga kuiwezesha Afrika katika sekta ya uchumi na uwekezaji. Ili kufikia lengo hilo, mkutano huo umewashirikisha wadau wa sekta binafsi zikiwemo kampuni binafsi zaidi ya 300 kutoka Japan. 

Katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu, Rais wa kampuni ya Sumitomo, Bw. Kuniharu Nakahura, alisema kampuni hiyo imeanza utekelezaji wa mradi wa Kinyerezi II wa kuzalisha umeme wa MW240 kutoka gesi asilia (Gas Fired Combined Cycle Gas Power Plant). Mradi huo ulioanza kutekelezwa Machi 2016, unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu.

Bw. Nakahura ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, alisema kampuni yao inajishughulisha zaidi na utengenezaji wa bidhaa za vyuma, kemikali, ujenzi wa miundominu, na usafirishaji. 

Naye Makamu wa Rais wa kampuni ya Toyota Tshuso, Bw. Yasuhiko Yokoi alikutana na Waziri Mkuu na kumweleza jinsi kampuni hiyo kubwa duniani inavyoweza kushiriki na kuchangia maendeleo nchini Tanzania.

Alisema kampuni yao inajishugulisha zaidi na masuala ya miundombinu ikiwemo kuzalisha mitambo ya umeme na mitambo ya bandari. Pia inazalisha bidhaa za kilimo (matrekta, mashine za viwanda vya mbolea na nguo, ujenzi wa maghala ya nafaka), mitambo ya nguvu za umeme wa joto-ardhi na uzalishaji wa magari ya aina mbalimbali.

“Kwa mfano hapa Kenya, tumeweza kutengeneza mitambo midogo ya kisasa ambayo inazalisha mbolea tofauti kulingana na hali halisi ya udongo wa mahali husika. Huwezi kuzalisha mbolea ya aina moja na kuamua kuisambaza kwa nchini nzima. Tunapima udongo wa sehemu moja na kuzalisha mbolea inayofaa kwa udongo ule,” alisema.

Naye Rais wa kampuni ya Marubeni, Bw. Fumiya Kokubu alimweleza Waziri Mkuu kwamba maeneo ambayo wangependa kuwekeza ni kwenye viwanda vya nguo, mbolea, saruji, uzalishaji wa sukari, umeme wa gesi na hasa miradi ya LNG. 

Kwa upande wake, Waziri Mkuu aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa Serikali iko tayari kushirikiana nao na akawashauri watume timu za maafisa wao ili wakutanishwe na wadau wa sekta husika.

Alisisitiza kuwa Tanzania hivi sasa imedhamiria kuwa nchi ya uchumi wa viwanda na kwa sababu hiyo inahitaji kuwa na nishati ya kutosha ili iweze kumudu kuendeleza sekta hiyo. “Serikali ya awamu ya tano imeamua kujenga uchumi wa viwanda, tunahitaji kujenga viwanda vya kutosha ili tuweze kusindika mazao ya wakulima ambao wanafikia asilimia 80 ya Watanzania wote. Tunahitaji masoko ya uhakika kwajili ya mazao wanayozalisha,” alisema.

Akiwa kwenye mkutano huo, Waziri Mkuu pia alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya wakimbizi, Bw. Filippo Grandi; Meya wa Jiji la Yokohama, Bibi Fumiko Hayashi; na Makamu wa Rais wa Kwanza wa Sudan, Jenerali Bakri Hassan Saleh.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu alitembelea Maonesho ya Biashara ya Afrika na Japan (Africa-Japan Expo 2016) ambapo Mamlaka ya Kuendeleza Biashara Tanzania (TANTRADE) na wadau wengine kama Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) walishiriki.

Akiwa huko alitembelea pia mabanda ya Uganda, Rwanda, Sénégal, Kenya, Japan na UN Habitat. Pia alitembelea banda la wajasiriamali wa nguo kutoka Tanzania ambao walishiriki maonyesho hayo yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Jomo Kenyatta (JICC) jijini Nairobi, Kenya.
Waziri Mkuu alirejea jijini Dar es Salaam jana usiku.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.

JUMATATU, AGOSTI 29, 2016.