WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekipiga marufuku Chuo Kikuu Ardhi kukodi makampuni ya kufanya kazi mbalimbali kwa niaba yake, akisema kuwa kitendo hicho kinaharibu kazi na sifa ya chuo hicho kwa kuwa baadhi ya makampuni wanayoyapa kazi hayakidhi vigezo.

Waziri Mkuu  ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Novemba 23, 2017) kwenye ufunguzi wa sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya Chuo Kikuu Ardhi.

“Kama kuna umuhimu wa kufanya kazi na kampuni ni bora muanzishe kampuni ya kwenu itakayofanya kazi vizuri ili kujiepusha na matatizo," amesema na kukiagiza chuo hicho kufanya tafiti zenye kuleta majibu ya maswali na changamoto mbalimbali zinazolikabili Taifa na Dunia. Ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni mabadiliko ya tabia nchi, ujenzi holela, uharibifu wa mazingira na majanga ya asili kama mafuriko. 
Amesema Serikali inaamini kuwa matokeo ya kazi zinazofanywa na chuo hicho zikiwemo tafiti ni chachu ya maendeleo ya taasisi za elimu ya juu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Dira ya Maendeleo ya Taifa imeweka mkazo wa kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kupato cha kati ifikapo 2025, hivyo wanahitajika wataalamu wa kutosha na wenye weledi.

“Hivyo Chuo Kikuu cha Ardhi kama taasisi ya Serikali inawajibu mkubwa wa kutayarisha wataalamu mbalimbali wa sekta za ujenzi, ukadiriaji majenzi na uhandisi wa mazingira," amesema Waziri Mkuu na kukitaka chuo kitumie fursa hiyo ya kuadhimisha miaka 10 ya chuo hicho kujitafakari na kuona ni kwa namna gani wanaweza kuwekeza zaidi ili kuongeza tija ya uwepo wa taasisi hiyo kwa jamii na Taifa kwa ujumla. 
“Wekeni mikakati madhibuti itakayowezesha chuo kupiga hatua kubwa zaidi katika kipindi cha miaka 10 ijayo. Siku zote mjikite katika kutafuta kuwa na ubora zaidi ya wakati uliopita," alisisitiza. 
Awali, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema Serikali inakkitegemea chuo hicho katika kufanikisha ajenda yake ya uchumi wa viwanda kwa kuwa kinatoa wataalamu wengi. 
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Mkuu wa chuo hicho ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa David Msuya, Mwenyekiti wa Baraza la chuo Bibi Tabitha Siwale, Makamu Mkuu wa chuo Profesa Evaristo Liwa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, wanafunzi na watumishi wa chuo hicho.
 Waziri Mkuu Mhe. Kassim Malijaliwa (kulia) akisalimiana na Waziri Mkuu Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu cha  Aridhi Tanzania Mhe. David Cleopa Msuya wakati wa uzinduzi wa Sherehe ya miaka Kumi ya Chuo Kikuu cha Ardhi ambayo yameanza leo Novemba 23/2017 Jijini Dar es salaam.
Waziri Mkuu mhe Kassim Majaliwa akiongea na Makamu Mkuu wa Chuo cha Ardhi Profesa Evaristo Liwa (kulia) na Waziri wa Elimu,Sayansi,Teknolojia na Ufundi. Profesa Joyce Ndalichako wakati wa ufunguzi wa Sherehe za Miaka 10 ya Chuo cha Ardhi jijini  Dar es salaam. 
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...