WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameongoza viongozi kadhaa na baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuuaga mwili wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Bw. Moshi Chang’a ambaye alifariki dunia Aprili 20, 2014 kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alikuwa akipatiwa matibabu. 
 Shughuli ya kuuaga rasmi mwili wa marehemu Chang’a kwa wakazi wa mji wa Dar es Salaam ilifanyika leo mchana (Jumanne, Aprili 22, 2014) nyumbani kwake Mbagala, Kibonde Maji, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. 
Mwili wake utasafirishwa leo jioni kwenda Kihesa, mkoani Iringa kwa mazishi. Akizungumza na waombolezaji hao kabla ya kutoa heshima za mwisho, Waziri Mkuu Pinda alisema amemfahamu Bw. Chang’a kwa muda mrefu kwa sababu sehemu kubwa ya utumishi wake ameifanya akiwa Serikalini. 
 “Ninyi mlimfahamu Bw. Chang’a kivingine lakini mimi nilimfahamu kwa namna ya tofauti kutokana na jinsi alivyokuwa msaada mkubwa kwa Serikali kila tulipokuwa tukipata shida ama migogoro ya kiuongozi.”
 “Kama TAMISEMI, tumemtumia sana kusawazisha mambo kwa sababu Mungu alimjalia kipaji cha pekee ambacho ni ucheshi... hata jambo lingekuwa gumu vipi, huyu Bwana alijua kufikisha ujumbe bila kumuudhi mhusika kutokana na maneno yake,” alisema Waziri Mkuu. 
 Alitumia fursa hiyo kufikisha salamu za rambirambi kwa wafiwa kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye yuko safarini kikazi. 
 Vilevile, aliwataka wanafamilia ambao wamebaki bila mama wala baba, wawe na umoja na mshikamano na kuahidi kuwa Serikali itawasaidia watoto wa marehemu wakamilishe malengo ya elimu yao kama ambavyo baba yao alikuwa amepanga. 
 Marehemu Chang’a anatarajiwa kuzikwa kesho (Jumatato, Aprili 23, 2014) huko Kihesa, Manispaa ya Iringa ambapo Serikali itawasilishwa na Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI), Bibi Hawa Ghasia. Marehemu ameacha watoto watano, wa kike watatu na wa kiume wawili. 
 IMETOLEWA NA: 
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
S. L. P. 3021, 
DAR ES SALAAM 
JUMANNE, APRILI 22, 2014
  Waziri Mkuu Mizengo Pinda akitoa pole kwa waombolezaji kabla ya kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Marehemu Moshi Chang'a, nyumbani kwa Marehemu Mbagala Kibonde Maji jijini Dar es salaam leo Aprili 22, 2014. Kushoto ni mkewe Mama Tunu Pinda.
Waziri Mkuu na Mkewe Mama Tunu  Pinda wakitoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Marehemu Moshi Chang'a, nyumbani kwa Marehemu Mbagala Kibonde Maji jijini Dar es salaam

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...