Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga akiwatambulisha watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (Mb) alipoitembelea ofisi hiyo mapema leo.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (Mb) akisisitiza uwajibikaji kwa watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) alipoitembelea ofisi hiyo mapema leo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (Mb) akiagana na viongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mara baada ya kumaliza ziara ya kikazi aliyoifanya Makao Makuu ya TASAF mapema leo. 

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais ,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (Mb) ameuagiza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kusaidia jitihada za serikali za kuwaondolea wananchi kero ya umaskini.

Mhe. Kairuki amesema TASAF inayo dhima kubwa ya kuhakikisha kuwa huduma inazozitoa kwa wananchi zinakwenda sambamba na misingi ya uadilifu na utawala bora ili hadhi ya mfuko huo iendelee kuwa kubwa. 

Waziri Kairuki ameyasema hayo alipotembelea Makao Makuu ya TASAF jijini Dar es salaam ambako alizungumza na watumishi wa mfuko huo ikiwa ni mwendelezo wa ziara za kikazi katika taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora ambayo amepewa dhamana ya kuisimamia baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John P. Magufuli.

“Ninawasisitiza muhakikishe kuwa, walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wananufaika vilivyo na fedha zinazotolewa ili hatimaye waweze kuondokana na umaskini” alisema Kairuki.

Aidha, Mhe. Kairuki ameuagiza uongozi wa TASAF kuweka utaratibu utakaowezesha ukaguzi wa mara kwa mara wa walengwa wa Mpango huo nchini kote ili kuhakikisha kuwa watu wasiostahili wanaondolewa kwenye utaratibu wa ruzuku na kupunguza malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

Mhe. Kairuki ameonya vikali dhidi ya uwezekano wa kuweko matumizi mabaya ya fedha kwa kutoa ruzuku kwa watu wenye uwezo jambo ambalo amesema halipaswi kufumbiwa macho na pale itakapobainika wahusika wachukuliwe hatua za kuwaondoa kwenye Mpango na kisha kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki ameuagiza uongozi wa TASAF kutoa mapendekezo ndani ya siku 30 ya namna ya kukabiliana na malalamiko yanayoelekezwa kwa watendaji wa ngazi za vijiji,kata,na hata wilaya ambao wamekiuka taratibu za kuwabaini na kuwaorodhesha walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya maskini ili hatua zichukuliwe haraka iwezekanavyo.

Awali akitoa maelezo kwa Waziri, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bw. Ladislaus Mwamanga amesema Mfuko umefanikiwa kuandikisha zaidi ya walengwa Milioni 1.1 ambao wanaendelea kupata ruzuku na kuwa hadi kufikia mwezi Januari 2016 zaidi ya shilingi Bilioni 204 zimetolewa kwa walengwa ambapo matokeo chanya yameanza kuonekana hususani katika Nyanja za elimu, afya na makazi.

Bwana Mwamanga amesema licha ya changamoto zilizopo hususani katika upatikanaye wa fedha za kukidhi idadi kubwa ya walengwa ,Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF )umeendelea kufanya juhudi za kutafuta fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo na kuiomba serikali kuona namna inavyoweza kuunga jitihada hizo ili hatimaye vita dhidi ya umaskini iweze kufanikiwa .

Kuhusu Mpango wa kunusuru kaya maskini, Bw. Mwamanga amesema walengwa wa Mpango huu wamehamasika kwa kiwango kikubwa huku wengi wao wakionyesha uwezo katika kufuata masharti na taratibu za Mpango hivyo suala la upatikanaji wa fedha kwa uhakika lina umuhimu mkubwa ili kutowavunja moyo walengwa hao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...